Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC Clatous Chotta Chama amesema yupo tayari kuikabili Tanzania ‘Taifa Stars’ katika mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Michuano ya Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ utakaopigwa Jumapili (Januari 21).
Taifa Stars itaikabili Zambia katika mchezo huo ambao utakuwa na maamuzi kwa taifa hilo la Afrika Mashariki ya kuona kama itaendelea kuwa sehemu ya timu zitakazokuwa na nafasi ya kutinga Hatua ya Mtoano, baada ya kupoteza mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza dhidi ya Morocco, uliopigwa jana Jumatano (Januari 17).
Chama ambaye hakucheza katika mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza dhidi ya DR Congo uliomalizika kwa sare ya 1-1 jana Jumatano (Januari 17), amesema endapo Kocha Avram Grant atampa nafasi ya kuikabili Tanzania atakuwa tayari kupambana kwa ujasiri ili kuipa matokeo timu yake.
Amesema anafahamu mchezo huo utakuwa mgumu, lakini anaamini timu itakayokuwa bora itakuwa na nafasi ya kuondoka na alama tatu muhimu, hivyo kila upande unapaswa kujiandaa.
“Nipo tayari kuikabili Tanzania kama Kocha akinipatia nafasi, ni bahati mbaya kuwa sijacheza katika mchezo wetu dhidi ya DR Congo, ikitokea nimepangwa katika mchezo unaofuata nitaipambania timu yangu.
“Ninaifahamu Tanzania kwa sababu ninafanya kazi yangu huko, ninawafahamu wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu ya Tanzania, kwa hiyo itakua rahisi kwa kila mmoja kumkabili mwenzake japo upande wetu sio wote tunaocheza katika Ligi ya Tanzania.” Amesema Chama.
Katika hatua nyingine Chama amesema bado Kundi F lipo wazi kwa timu yoyote kutinga kwenye Hatua ya Mtoano, licha ya Tanzania kuanza vibaya kwa kufungwa 3-0 dhidi ya Morocco, huku Zambia ikiambulia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya DR Congo.
“Kundi F bado lipo wazi, timu yoyote inaweza kutinga Hatua ya Mtoano, kupoteza kwa Tanzania katika mchezo wake wa kwanza haimaanishi ndio safari imeishia hapo, inaweza kufanya vizuri katika michezo inayofuata na ikasonga mbele.”
“Hata Zambia nayo ina nafasi kama ilivyo kwa DR Congo na Morocco ambayo kwa sasa inaongoza msimamo wa Kundi letu, kwa hiyo mchuano bado ni mgumu, na ni mapema sana kuanza kusema nani atakuwa sehemu ya timu mbili zitakazofuzu Hatua inayofuata.” amesema