Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wamesema wana matumaini makubwa na maingizo mapya ya wachezaji waliowasajili dirisha dogo, msimu huu 2023/24.
Wachezaji waliosajiliwa ni Shekhan Ibrahim kutoka JKU ya Zanzibar, Agustine Okrah kutoka Benchem ya Ghana na Joseph Guede aliyesajiliwa dakika za mwisho kutoka Uturuki.
Young Africans pia iliachana na Jesus Moloko huku ikiwatoa kwa mkopo Crispin Ngushi kwenda Coastal Union na Hafiz Konkoni kwenda klabu moja ya Cyprus.
Akizungumza Dar es salaam, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Young Africans anga, Ali Kamwe amesema usajili huo wa wachezaji watatu umezingatia mapendekezo ya benchi la ufundi kwa kuimarisha kikosi chao.
Kamwe amesema ni vigumu kuwapata wachezaji wazuri katika dirisha dogo la usajili lakini wao wamefanikiwa na kupongeza juhudi za Rais wa klabu hiyo Hersi Said, kufanikisha matakwa ya benchi la ufundi.
“Tumeongeza wachezaji wapya kwa kufuata matakwa ya benchi la ufundi, tuupongeze uongozi kwa kufanikisha hili, kwani sio jambo rahisi kuwapata wachezaji katika kipindi hiki lakini tumewapata,” amesema.
Tayari Young Africans imeanza mazoezi Avic Town, Dar es salaam kujiandaa na mechi za Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.