Kocha Mkuu wa Mali, Eric Chelle amesema kikosi chake hakiwezi kuchukuliwa moja ya timu zinazopewa kipaumbele kushinda ubingwa wa fainali za mataifa ya Afrika pamoja na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Afrika Kusini.

Mali walioanza mchezo taratibu walirudi wakiwa imara kipindi cha pili na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Afrika Kusini.

Akizungumza baada ya mchezo huo mjini Korhogo, Chelle alisema ana furaha na ushindi huo lakini aliwaonya wahezaji wake wasibweteke na ushindi huo na kuongeza bado wanakabiliwa na mechi mbili kukamilisha hatua ya makundi.

“Nataka kuwapongeza wachezaji kwa ushindi huu. Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri. Tulikuwa kwenye presha. Kipindi cha pili tuliongeza kasi. Tulisababisha Penati, kama wangefunga habari pengine ingekuwa tofauti,” alisema Chelle.

“Kila taifa lina nafasi yake na mashindano haya yanavutia sana kwa sababu timu zina ubora. Siwezi kusema kama tuna nafasi kubwa kuvuka kundi.

“Ndio, tumepata ushindi, lakini mengi bado yanaweza kutokea. Bado tuna mechi za kucheza na tunatakiwa kuendelea kupambana,” amesema Chelle.

Mali inaongoza Kundi E kwa kuwa na uwiano mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kuwazidi Namibia waliopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tunisia.

Wachezaji wapya Simba SC mtegoni
Wanafunzi watakiwa kuvunja ukimya matukio ukatili