Wanafunzi wa Shule ya Msingi Izia iliyopo Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa, wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, kwa kuvunja ukimya dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa kitengo cha Dawati la jinsia na watoto Manispaa ya Sumbawanga, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Hatimu Tabia alipofika shuleni hapo kutoa elimu ya Ukatili wa Kijinsia na athari za matumizi ya dawa za kulevya.
Tabia amesema matumizi ya dawa za kulevya husababisha kudumaa kwa akili hali inayosababisha mtu kupatwa na matatizo ya afya ya akili na kushindwa kuendelea vyema kimasomo.
Aidha, Mkaguzi Tabia alizitaja pia athari za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kuwa ni kupata mimba za utotoni, kukatisha masomo, kupata magonjwa ya kuambukizwa, kuwa na familia tegemezi, kujiunga katika makundi ya uhalifu, kuwepo na wimbi la watoto wa mitaani na kuwa wahalifu.