Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa, Karim Benzema amewasilisha kesi mahakamani ya kuharibiwa jina dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa kwa kumtuhumu ana uhusiano na Kundi la Muslim Brotherhood, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti.
Waziri, Gérald Darmanin, alisema mnamo Oktoba, mwaka jana Benzema “ana uhusiano mbaya” na Kundi la Kiislamu la Sunni.
Maoni hayo “yanadhoofisha” heshima na sifa yake, wakili wa Benzema alisema.
Kundi la Muslim Brotherhood limepigwa marufuku katika nchi kadhaa zikiwamo Misri, Urusi na Saudi Arabia.
Maoni ya Darmanin ya Oktoba yalikuja baada ya mchezaji huyo kuandika kwenye ukurasa wake wa Twitter anaunga mkono watu wa Gaza kama “waathiriwa tena wa mashambulizi ya kidhalimu ya mabomu ambayo hayawaachi wanawake wala watoto”.
Alisema Benzema alishindwa kuonyesha huruma kama hiyo kwa waathirika 1,300 wa Israel waliouawa na Hamas Oktoba 7, mwaka jana.
Darmanin alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Ufaransa “anajulikana sana kwa uhusiano wake na Muslim Brotherhood”.
“Tunapambana na zimwi ambalo ni Muslim Brotherhood, kwa sababu inajenga mazingira ya jihadi,” mwanasiasa huyo alikiambia kituo cha televisheni cha kihafidhina cha CNews.
Benzema mwenye umri wa miaka 36, ambaye anacheza Saudi Arabia na alikanusha haraka madai hayo na kutishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waziri huyo kwa kashfa.