Kiungo mpya wa Simba SC, Babacar Sarr amerejea kwao Senegal ili kuweka mambo sawa, huku akisema tayari ameshakisoma kikosi hicho kipya na akirudi kazi aliyonayo ni moja tu kukiwasha.
Sarr aliyesajiliwa katika dirisha dogo na kuanza kukitumikia kikosi kwenye mechi mbili za michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024, ambapo Simba SC ilifika fainali na kupoteza kwa bao 1-0 mbele ya Mlandege, huku akishindwa kuonyesha makali na kuzua maswali kwa mashabiki, lakini mwenyewe amewatuliza.
Akizungumza kabla ya kuondoka nchini, Sarr mwenye kibarua cha kuchuana na viungo aliowakuta kikosini kina Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma na Abdallah Hamis amesema anarudi kwao kuweka kila kitu sawa kwani alikuja nchini ghafla kwa ajili ya usajili, lakini ameshasoma mchezo.
Amesema anajua ana kibarua kigumu ndani ya Simba SC, hivyo anaenda kuweka mambo sawa baada ya kupewa mapumziko na anaamini akirudi atakuwa na kazi moja tu ya kujituma mazoezini kabla ya kuanza kufanya kazi Uwanjani akiamini mashabiki wana kiu naye.
“Mechi mbili nilizocheza kwangu zimenifundisha vingi, ila kubwa ni kukisoma kikosi na nimefanikiwa kwenye hilo sasa hesabu ni moja tu namna ya kupata namba kwani wachezaji wote wako vizuri na wana uwezo mkubwa.” amesema Sarr aliyewahi kukipiga US Monastir ya Tunisia.
“Ninachokipambania ni kuelewana na wachezaji wenzangu kwa haraka ili tuelewana namna ya kucheza kwa urahisi, lakini sina shaka na uwezo wangu japo bila juhudi kuanzia mazoezini ndizo zitanifanya kupata namba kirahisi na kocha kuniamini.”
Kati ya wachezaji anaocheza nao nafasi moja ni Mzamiru tu ndiye hajamuona, kwa vile yupo timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, huku waliosalia alikuwa nao katika michuano ya Mapinduzi iliyomalizika kwa Mladenge kutetea taji kwa mara pili mfululizo.