Baada ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Cape Verde kwenye mchezo wa Kundi B wa michuano ya fainali za mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, baadhi ya mashabiki wa Ghana wana imani timu yao inaweza kupata ushindi kwenye mchezo wa leo Alhamis (Januari 18) dhidi ya Misri.
Cape Verde waliishtua Ghana kwa kipigo cha mabao 2-1 Jumapili (Januari 14) na kuongoza kundi hilo wakiwa na pointi tatu huku Ghana wakishika mkia.
Misri na Msumbiji kwa pamoja wanashika nafasi ya pili baada ya kutoka sare ya bao 2-2 kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi B.
Wakionekana kutosumbuliwa na matokeo hayo ya mchezo wa kwanza, baadhi ya mashabiki wa Ghana waliopo Abidjan wanaamini timu yao itapata ushindi dhidi ya Misri na kuweka matumaini yao hai ya kuingia hatua ya mtoano ya michuano hiyo.
Huku timu hiyo ikiwa na kawaida ya kuanza taratibu mashindano hayo, mashabiki hao wanaamini Ghana maarufu kama Black Stars wanaweza kupata pointi tatu dhidi ya Misri.
Akizungumza na vyombo vya habari Kwame Owusu, amesema kama timu yao itapangwa vizuri, ana uhakika wataifunga Misri na kuingia hatua ya mtoano.
Tunaweza kupata pointi tatu dhidi ya Misri na vilevile dhidi ya Msumbiji na kufuzu. Timu inaweka mambo sawa wakati huu,” amesema.
Mpiga ngoma mkuu wa mashabiki wa timu hiyo, Joseph Langabel aliyewalaumu wachezaji wa timu hiyo kwa matokeo ya mchezo uliopita, amesema wakati wote kuna nafasi ya kubadilika.
“Aina hii ya mpira wa Ghana haikubaliki. Wanacheza kama hakuna kitu wanashindania na mwisho wanatuvunja moyo,” amesema.
“Hakika wanatakiwa kufanya vizuri mchezo unaofuata, kinyume chake hatutafuzu kuingia hatua ya mtoano ya mashindano haya,” amesema.
Afua Serwaa, aliyetarajia kusumbua mitaa ya Ivory Coast kushangilia ushindi wa Ghana amesema:”Nina hakika kutakuwa na ushindi kwenye mechi zetu zinazofuata. Tunatakiwa kuwaamini wachezaji wetu walete matokeo mazuri.
“Dede Ayew na wenzake wanatakiwa mechi inayofuata kufidia machungu tuliyopata,” amesema.
Wakati huo huo, wakielezea matumaini yao kuelekea mechi inayofuata, mashabiki hao walivamia mgahawa wa Maquis Du Val kushangilia.
Wakiwa zaidi ya 100 waliimba nyimbo za kabila la Jama na kucheza ngoma za asili za baadhi ya makabila ya Ghana.