Mshambuliaji wa Klabu Bingwa nchini Italia SSC Napoli, Victor Osimhen, amethibitisha nia yake ya kutaka kucheza katika Ligi Kuu England (EPL), kwa siku zijazo, lakini amesisitiza kujitolea kwake kwa timu yake ya sasa.
Osimhen analengwa kwa muda mrefu na Chelsea, ambayo inatafuta suluhisho ya matatizo yao ya ufungaji kwa mwaka huu, huku Arsenal pia ikihusishwa kumtaka mchezaji huyo wa kimataifa wa Nigeria, ambaye hivi karibuni alisaini mkataba mpya na SSC Napoli, ambao unajumuisha kipengele cha kutolewa chenye thamani ya zaidi ya Pauni Milioni 100.
Kuongezewa kwa mkataba wake kulionekana kutokuwa na uhakika mwanzoni mwa msimu huu wakati Osimhen alipotumiwa ujumbe wa matusi katika mtandao wa kijamii kutoka akaunti ya SSC Napoli, lakini mvutano ulimalizwa na Osimnhen akasaini mkataba mpya.
“Nina furaha na Rais wa SSC Napoli,” alisema Osimhen akiiambia Sky Sport.
“Nina uhusiano mzuri naye, siwezi kusema uongo, amekuwa nami tangu niliposaini katika klabu hii mwaka, 2020.
“Nina uhusiano mzuri na familia yake pia. Siku zote ni muhimu kwangu kuhakikisha hakuna kitu kibaya, bila kujali kilichotokea na uhusiano na yeye na familia yake.
“Amekuwa akiniunga mkono nje ya uwanja na bila shaka najitolea kwa bidii kushinda Scudetto nikiwa nao.”
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuhamia England, Osimhen alikiri: “Ni kweli siku moja, bila shaka, lakini kwa sasa nina mipango mingine katika kazi yangu. Wakati utakapofika, kila mtu atajua.”
Osimhen hapo awali alikiri alikuwa na jezi za Chelsea na Manchester United alipokuwa mtoto, ingawa alikataa nafasi ya kusajiliwa na Mashetani Wekundu mwaka 2020.
Sasa akiwa mmoja wa washambuliaji bora duniani, Osimhen anawaniwa na klabu nyingi, lakini bei yake bila shaka itapunguza timu ambazo zinaweza kufanya makubaliano ya kumsajili.
Chelsea wanatarajiwa kuendelea na harakati zao za kumnasa Osimhen baada ya dirisha dogo la usajili la Januari, huku Arsenal pia wakitafuta chaguo lao la mshambuliaji.