Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke – TRRH, inatarajia kuweka kambi na kutoa huduma za matibabu na kiuchunguzi wa kibingwa na bingwa bobezi katika kituo cha Afya cha Buza kwa rnuda wa siku tano, kuanzia Januari 22 – 26, 2024.
Taarifa iliyotolewa na Afisa Uhusiano na mawasiliano kwa Umma, Cleopatra Mokiwa imeeleza kuwa Kambi hiyo, itahusisha Huduma za kiuchunguzi na matibabu ya kibingwa na bingwa bobezi katika maeneo mbalimbali ya afya, kama vile magonjwa ya ndani, macho, pua, masikio na koo (ENT).
Taarifa hiyo imeyataja matibabu mengine kuwa ni kinywa na meno, huduma za wanawake na uzazi, upasuaji, mifupa, afya ya akili, upasuaji wa njia ya mkojo, utengamao, huduma za watoto pamoja na zoezi la uchangiaji damn wa hiyari.
Aidha, uwepo wa kambi hiyo ya matibabu ni mojawapo ya mikakati ya Hospitali katika kuhakikisha huduma za kibingwa zinawafikia moja kwa moja wananchi kwa kutambua umuhimu wa afya bora katika kuboresha maisha ya jamii.