Mshambuliaji Hafiz Konkoni anayejiandaa kuondoka nchini kwenda kujiunga na timu ya Dogan Tùrk Birligi ya Cyprus kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu 2023/24 akitokea Young Africans, amefichua kwamba, anawaona mabingwa hao wa nchi, wakifika mbali katika mechi za kimataifa, huku akiichomoa Simba SC akidai labda itokee tu.
Konkoni aliyesajiliwa na Young Africans msimu huu akitokea Bechemn United ya Ghana kwa lengo la kuziba pengo lililoachwa na Fiston Mayele aliyepo kwa sasa Pyramids ya Misri, alishindwa kupata namba katika kikosi cha kwanza, kabla ya uongozi kuamua kumtoa kwa mkopo Birligi kupitia dirisha dogo lililofungwa juzi Jumatatu.
Akizungumza kabla ya kuondoka jijini Dar es salaam, Konkoni amesema anasikitika kuachana na Young Africans katika kipindi hiki, kwani alikuwa anaiona nafasi yake kikosini kama angeendelea kuaminiwa, lakini kwa vile imeshatokea hana budi kukubali, huku akiitabiria pia kufanya makubwa.
Konkoni amesema Young Africans inaundwa na wachezaji wenye viwango bora na wanaojituma uwanjani, ndio maana hata yeye alikuwa akipata ugumu kupenya kikosi cha kwanza na kwamba anaiona timu hiyo ikifika mbali zaidi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kulinganisha na watani wao wa jadi, Simba SC.
“Niwe muwazi kuwa Young Africans ina kikosi kizuri na wachezaji bora, naiona ikifika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kuliko Simba SC, kwani Young Africans ina wachezaji wazuri sawa na Simba SC, ila tofauti yao ni moja tu fitnesi.
Young Africans ina fitnesi ya hali ya juu kuliko Simba SC. Lakini mpira una maajabu yake wote nawatakia heri kwenye mashindano hayo,” amesema Konkoni.
Mshambuliaji huyo aliongeza, anaondoka Young Africans akiwa anaipenda na deni kubwa la kushindwa kutimiza malengo ya usajili.
“Haukuwa muda sahihi kwangu kuondoka Young Africans, bado nina deni kubwa kwa mashabiki kwa vile sikupata nafasi ya kuitumikia vya kutosha, lakini sina namna.
Nimeshaenda kuwaaga wachezaji wenzangu pamoja na kocha na kuitakia kila la kheri wakati najiandaa kwenda kuanza maisha mapya katika timu nitakayoitumikia.”
Hadi anaondoka Young Africans, Konkoni ameifungia timu hiyo mabao mawili tu, likiwamo moja la Ligi Kuu Bara katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya KMC na jingine kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asas ya Djibouti iliyofumuliwa mabao 5-1.
Nafasi ya mchezaji huyo mrefu imezibwa na mshambuliaji mpya Joseph Guede kutoka Ivory Coast aliyetambulishwa muda mfupi kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Junatatu usiku, akiwa ni mchezaji wa pili baada ya Mghana Augustine Okrah aliyechukua nafasi ya Jesus Moloko aliyeachwa.