Halmashauri ya Chama cha Mapinduzi – CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, imepokea taarifa ya Miradi ya maendeleo ya Mkoa huo, inayotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), na Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD), inayoendelea kutekelezwa, ukiwemo mradi wa Bonde la Mto Msimbazi, Ujenzi wa Daraja la juu la jangwani, hali ya Barabara zilizoathiriwa na Mvua na mpango wa Serikali katika karabati hizo.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvuukiwa pia kililenga kututatua changamoto ya Madawati katika shule mbalimbali ambazo zilizo na uhaba, ukiwa ni kutekeleza sera ya Chama cha Mapinduzi ya kutoa elimu bure kwa Wanafunzi wote, kuanzia ngazi ya awali hadi Sekondari.
Miradi hiyo, mingi imekamilika kwa kiwango kikubwa cha utekelezaji wake katika awamu ya kwanza ambapo sasa mikakati kazi ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa DMDP unatarajiwa kuanza mwezi Mei 2024, ambao utajielekeza zaidi kwenye kujenga baadhi ya Barabara kuu na za mitaa katika Wilaya zote za jiji.
Aidha, kikao hicho pia kililenga kutatua kero zinazotokana na athari za mafuriko eneo la Jangwani, kulipa fidia Kwa waathirika wa mradi, kuzuia mmomonyoko, utunzaji wa maji, kurudisha uoto wa asili, kuweka mifumo ya kuruhusu maji kwenda baharini, kuweka mpango mji vizuri eneo hilo, kudhibiti athari ziyokanazo na taka ngumu pamoja na usimamizi wa bonde.
Akifafanua kuhusu hali ya mradi huo, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa DMDP, Nyariri Nanai amesema gharama za mradi zinatarajiwa kuwa dola 438 Milioni ambazo zinafadhiliwa na Benki ya Dunia pamoja na ruzuku ya Serikali ya Uholanzi, huku Wakandarasi wenye sifa wakitakiwa kuomba tenda hizo pindi zitakapotangazwa Februari 2024.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Wenyeviti wa CCM wa Wilaya zote za Dar es Salaam, Makatibu wa CCM Wilaya, Mameya wa Wilaya, Mkurugenzi wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Wataalamu na Mameneja Miradi wa TANROAD, wadau mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na Waandishi wa Habari.