Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Honoratha Rutatinisibwa amefungua mafunzo ya Kadi Alama (Community Score Card) ya kutathmini utoaji wa Huduma za Afya ya Mama na Mtoto ili kupunguza Vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Akifungua mafunzo hayo Mkoani humo, Dkt. Rutatinisibwa amewataka washiriki hao kushiriki kikamilifu ili kuongeza uelewa na kuboresha huduma za afya na kuondoa malalamiko kutoka kwenye jamii kwa kuwa serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye sekta ya afya.
Amewaasa washiriki hao kufuatilia mafunzo hayo ili kujua kadi alama ya jamii inayoruhusu jamii inayotumia huduma hizo kufanya tathmini pamoja na watoa huduma wa Kituo husika ili kubaini changamoto na kuzitafutia suluhisho kwa kushirikiana na jamii husika.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Jesca Mugabiro amesema mafunzo hayo yanalenga kusimamia uwajibikaji wa watumishi waliopo kwenye Vituo vya kutolea Huduma za Afya kwenye Halmashauri na Mkoa kwa kuwa serikali imewekeza fedha nyingi kwenye Miundombinu ya Afya, ajira na Vifaa Tiba.
Naye, Mratibu wa Elimu kwa Umma kutoka Halmashauri ya Uyui, Robert Migango ameishukuru Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Afya kwa kupeleka mafunzo hayo mkoani Tabora ambayo yatasaidia kusimamia huduma za afya ya mama na mtoto.
Mradi mpya wa Tanzania Maternal and Child Health Investment Program (TMCIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unalenga kusaidia kuboresha utoaji wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto katika Vituo vya kutolea Huduma za Afya nchini kwa kutumia Kadi Alama ya Jamii ili kufanya tathmini ya Huduma husika.
Aidha, Mradi pia unalenga kuajiri Watumishi wa Kada mbalimbali wa Afya ambao watasaidia utoaji wa Huduma kwa jamii. Mradi huu umeanza kutekelezwa mwezi Desemba, 2022 na utatekelezwa kwa muda wa miaka Mitano hadi mwaka 2027.

NAM wazikutanisha Kampala theluthi mbili ya nchi Duniani
Joseph Geude: Wananchi mtafurahi