Licha ya kutokuwa na ingizo jipya kwenye dirisha dogo, Kagera Sugar imeendelea kujifua kambini katika mashamba ya miwa, mjini Bukoba huku wachezaji wakipewa kibarua kizito cha kuibeba timu hiyo.
Timu hiyo ilianza rasmi mazoezi tangu Januari 6, kwenye Uwanja wa Sobibo baada ya mapumziko ya siku 10, huku ikiwa haijafanya usajili wowote katika dirisha dogo lililofungwa Januari 15, licha ya kuwa katika nafasi ya tatu kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya mechi 13 ikivuna pointi 13 kwa kushinda michezo mitatu, sare nne na kupoteza sita, ikifunga mabao manane na kuruhusu l6.
Kocha wa timu hiyo, Marwa Chambeli aliyechukua nafasi ya Mecky Maxime aliyetupiwa virago Desemba 22, mwaka jana, amesema nyota wanaonyesha njia ya mafanikio kwa kutaka utofauti na kufika mbali.
Chambeli aliyewahi pia kuinoa Biashara United chini ya Francis Baraza, amesema kutokana na kujitambua kwa wachezaji, benchi la ufundi lina kazi moja tu ya kufanya katika kipindi hiki cha maandalizi kwa kuwataka wachezaji kujitambua, kujituma, kuipambania timu na kujitolea kuhakikisha timu inatoka katika nafasi za chini.