Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amekutana na kuzungumza na Wadau wa UNICEF, kujadiliana jinsi ya kuimarisha utekelezaji wa vipaumbele vya Sekta ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe .
Majadiliano hayo yaliyofanyika katika Ofisi za Idara ya Afya- TAMISEMI Dodoma, pia yalilenga kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendelea kuboresha Mifumo ya sekta ya Afya nchini hasa katika ngazi ya Huduma ya Afya ya Msingi.
Dkt. Mfaume alisema, Serikali inaendelea kuboresha Mifumo Stahimilivu ya sekta ya Afya na kwamba Ofisi ya Rais – TAMISEMI inalo jukumu la Kuratibu Utekelezaji wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na itahakikisha huduma bora kwa wananchi zinatolewa wakati wote katika Vituo vya Kutolea Huduma za Afya ngazi ya Msingi.
Naye Mkuu wa Seksheni ya Afya Shirika la UNICEF, Wendy Erasmaus amesema sekta ya Afya ni muhimu sana kwa wananchi na Shirika hilo linafurahi kufanya kazi na kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuendelea kuchangia utatuzi wa changamoto za sekta ya Afya, kuweka na kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watanzania.