Licha ya kuanza kwa kipigo kizito cha mabao 3-0 kwenye mchezo wa kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva ameweka wazi kuwa anaamini bado Taifa Stars ina nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano hayo kwa kushinda michezo miwili iliyobaki dhidi ya Zambia na DR Congo.
Taifa Stars juzi Jumatano (januari 17) ilianza vibaya kampeni yake ya ‘AFCON 2023’ baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Morocco kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi F, ambapo kutokana na matokeo hayo Stars inaburuza mkia kwenye kundi hilo.
Stars mara baada ya matokeo hayo sasa inajipanga na mchezo wa pili dhidi ya Zambia ambao unatarajiwa kufanyika Jumapili ya Januari 21, mwaka huu.
Msuva amesema, kwa sasa mchezo dhidi ya Morocco umeisha na wachezaji wanaamini bado wana nafasi ya kurekebisha makosa na kushinda mechi mbili zilizosalia.
“Tumepoteza mchezo wetu dhidi ya Morocco, lakini hatujapoteza mashindano bado tuna nafasi ya kurekebisha makosa na kusonga mbele.
Naamini benchi la ufundi limeona mapungufu ambayo yalijitokeza na tunakwenda kuyafanyia kazi naamini tuna nafasi ya kupata pointi sita mbele ya Zambia na DR Congo na tutafanya kila jitihada kupambana.”