Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera amesema usajili wa mshambuliaji, Meddie Kagere ndani ya kikosi hicho ni muhimu kutokana na kuondokewa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Reliants Lusajo aliyetua Mashujaa FC ya mkoani Kigoma.

Zahera amepongeza kitendo cha viongozi wa timu hiyo kuipata saini ya Mshambuliaji huyo kutoka nchini Rwanda, kwani anaamini pengo la Lusajo limezibwa ipasavyo kutokana na uzoefu wa Kagere katika mashindano mbalimbali hususan katika suala la ufungaji.

“Kila mmoja wetu anatambua umuhimu wa Lusajo ila kama kawaida mchezaji siku zote huwa anaangalia maslahi anayoona kwake yanamfaa, baada ya kuondoka tulifanya tathimini ya kina na kuona Kagere ni mbadala wake sahihi kikosini,” amesema.

Kuhusu mikakati ya kikosi hicho, Zahera amesema wamefanya maboresho kutokana na upungufu uliopo kwani hawakutaka tena kusajili wachezaji wengi ambao watakuwa hawana manufaa kikosini ndio maana waliboresha maeneo machache kwa usahihi.

Kagere aliyepita Simba SC na Singida FG akiwa amefunga bao moja msimu huu huku akifanya vizuri msimu uliopita wakati akikichezea kikosi hicho alipofunga mabao manane nyuma ya Mbrazili, Bruno Gomes aliyefunga 10.

Zahera alijiunga Namungo FC Desemba 30, akichukua nafasi ya Denis Kitambi aliyetua Geita Gold.

Msisitizo uimarishaji malezi ya familia wazidi kutolewa
Jeshi lavitahadharisha Vyuo vikuu