Mshambuliaji Charles Ilanfya, amefichua kilichomrejesha Mtibwa Sugar na kuamini mambo mawili yaliyochangia kufanya maamuzi hayo akitokea lhefu FC.
llanfya alikuwa akichezea Ihefu mwanzoni mwa msimu huu kabla ya kutimkia Mtibwa alikotoka kucheza msimu uliopita ambapo nako alitumika kwa msimu mmoja tu.
Nyota huyo wa zamani wa Mwadui FC, Simba SC na KMC FC amesema rekodi aliyoiacha Mtibwa Sugar ya kufunga mabao sita na asisti moja msimu uliopita ndio iliyomrejesha, Kwani akiwa Ihefu alifunga bao moja na kuasisti moja.
Mtibwa iliyopo nafasi ya 16 katika msimano wa ligi ikiwa na pointi nane baada ya kushinda mechi mbili na kupata sare mbili na kupoteza 10, imemsajili Ilanfya na nyota wengine ili kujiokoa na janga la kushuka daraja.
Mshambuliaji huyo mwenye nguvu amesema ukiacha rekodi hiyo ya msimu uliopita, lakini kiu ya kutaka kuiokoa Mtibwa isishuke daraja ni sababu nyingine, mbali na soka kuwa ajira na alikubali kurudi hapo ashirikiane na wenzake kuinusru timu hiyo.