Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Morocco, Walid Regragui amesema bao la kwanza lilikuwa muhimu kwenye mazingira magumu kwao na kwamba wamejifunza kutokana na makosa ya wengine.
Morocco walipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tanzania kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kundi F wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ inayoendelea Ivory Coast.
Nahodha wa timu hiyo, Romain Saiss alifunga bao hilo na kuwatanguliza Morocco iliyofika Nusu Fainali ya Kombe la Dunia huku Azzedine Ounahi na Youssef En Nesyri wakiongeza mengine mawili ndani ya dakika tatu baada ya kiungo wa Tanzania, Novatus Miroshi kuoneshwa kadi nyekundu.
“Mechi za kwanza wakati wote huwa ngumu na hali ya ukungu ilifanya kuwa ngumu zaidi, lakini tuliwaheshimu Tanzania,” alisema Regragui.
“Ari ya timu ilikuwa juu na tumepata ushindi muhimu. Tulitaka kufunga mapema na tulipata nafasi, lakini bao letu mwishowe lilitokana na mpira wa adhabu ndogo.
“Tulipofunga tu tukakamilisha sehemu ngumu ya mchezo. Kwa wakati fulani kipindi cha pili tulikubali tusiwe na mpira na kuutawala mchezo kama timu kubwa.”