Wananchi wametakiwa kuendelea kuimarisha malezi kwa familia na Watoto wao, ili kuwalinda na kuwaepusha kujiingiza katika vitendo vinavyoenda kinyume na maadili pamoja na kujihusisha matukio ya kihalifu jambo ambalo hupelekea kuwa na jamii yenye mmomonyoko wa maadili.
Kauli hiyo, imetolewa na Mkaguzi wa shehia ya Pangawe Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Hasnuu, wakati akizungumza na wananchi wa eneo hilo katika ziara yake ya kufanya vikao vya nyumba kwa nyumba ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi maalum wa “Familia yangu haina Mhalifu.”
Alisema, Wazazi na Walezi wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba watoto wanakuwa katika miongozo sahihi kwa kuwapa elimu za kiroho, ambazo zitawajenga kiimani na kujiepusha na makundi mabaya.
Aidha, alisisitiza ushiriki wa kamati za maadili katika kuwakutanisha Wazazi na Walezi wa Watoto wanaoonekana kujiingiza kwenye vitendo vinavyoenda kinyume na maadili, ili kutafuta suluhisho la changamoto kwa haraka.
Nao Wananchi wa shehia hiyo, wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kutekeleza Mradi wa “Familia yangu haina Mhalifu” ambao kwa kiasi kikubwa unatarajiwa kuwa suluhisho la vitendo vya kihalifu nchini.