Wamiliki wa Baa na Nyumba za kulala Wageni wametakiwa kutoa taarifa za Watoto wanaofikishwa katika sehemu zao za kazi kwa ajili ya kutumikishwa, pamoja na kuwafichua watu wenye tabia ya kuwaleta wanafunzi sehemu hizo kwaajili ya starehe, ili kutokomeza ajira, ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi yao.
Wito huo, unetolewa na Polisi Kata wa Kata ya Mwakakati, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Robert Philipo wakati akizungumza na baadhi ya wamiliki wa Baa na Nyumba za kulala Wageni wa kata hiyo.
Amesema, “ulinzi wa kuwalinda watoto na Wanafunzi unaanza na sisi makini kipindi hiki cha mwanzoni mwa mwaka, Wanafunzi wengi wamefungua shule na ndicho kipindi ambacho wanafunzi na watoto hutafutiwa kazi kutoka sehemu tofauti tofauti kwa kisingizio cha Wazazi/Walezi kukosa ada.”
“Sasa basi nawaomba mtoe taarifa kwa Jeshi la Polisi mara moja pindi uonapo swala hilo, ili nilishughulikie kwa haraka, pia hairuhusiwi kumpokea mtu aliye chini ya umri wa miaka 18 katika maeneo haya ili tutokomeze vitendo hivyo katika kata yetu,” alisema Mkaguzi Philipo.