Watu watano akiwemo Mtingwa Kilimanjaro maarufu kama Shetani (42), Mkazi wa Mbamba, wamefikiswa katika Mahakama ya Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza kwa shitaka la mauaji.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Tumsifu Barnabas Mwendesha mashtaka wa Polisi Mkaguzi wa Polisi, Martha Chacha amewataja washtakiwa wengine kuwa ni Majaliwa Damasi (18), Emmanuel Damasi (34), Selina Mchele (49) na Maneno Mashauri (19).
Washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Oktoba 12, 2023 huko Bukokwa Wilayani Sengerema, kwa kumuua Sophia Maduka (61) na mmewe Mathias Lusesa (73), wote wakazi wa Lwenge Wilayani humo kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Hata hivyo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote na kurejeshwa rumande kutokana na Mahakama hiyo kukosa Mamlaka kisheria ya kusiliza shauri hilo ambapo itakumbukwa kuwa taarifa ya kukamatwa kwa washtakiwa hao ilitolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP- Wilbroad Mutafungwa Januari 13, 2024.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi februari Mosi, 2024 kwaajili ya kutajwa tena.