Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Senegal, Aliou Cisse alipata matatizo ya kiafya, akawahishwa hospitalini kufuatia ushindi dhidi Cameroon, lakini sasa anaendelea vyema baada ya kupatiwa matibabu.

Simba wa Teranga waliendeleza mwanzo mzuri wa kutetea taji lao la Mataifa ya Afrika kwa ushindi wa mabao 3-1 na kutinga kibabe hatua ya 16 Bora.

Hata hivyo, Cisse alipata tatizo la kiafya na akapatiwa matibabu katika hospitali ya mjini Yamoussoukro ambako alilazwa usiku mzima.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 47 baada ya hapo aliruhusiwa kutoka hospitalini na kurejea kikosini kwake.

Taarifa ya shirikisho la soka la Senegal ilisema : “Vipimo alivyofanyiwa vimemhakikishia yuko sawa na amerejea kundini. Anaendelea vyema,”

Cisse amekuwa kocha wa timu ya taifa hilo tangu 2015 na aliongoza kutwaa ubingwa wa AFCON katika fainali za 2022.

Aliongoza pia katika fainali mbili zilizopita za Kombe la Dunia, zikiwamo za mwaka juzi kule Qatar ambako walitolewa na England katika hatua ya l6 Bora.

Ismaila Sarr, Habib Diallo na Sadio Mane walifunga mabao ya ushindi wakati Senegal ikiichakaza Cameroon, ambayo bao lake la kufutia machozi lilifungwa na Jean-Charles Castel letto.

Senegal itacheza mechi ya kukamilisha ratiba dhidi ya Guinea kesho Jumanne kabla ya kumsubiri mpinzani wa katika hatua ya 16 Bora.

Ukweli wa kutemwa Baleke, Phiri wafichuliwa
Ugonjwa 'Red Eyes' waathiri shughuli za kiuchumi