Kiungo na Nahodha wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England, Jordan Henderson ametua Ajax ya Uholanzi baada ya kumalizana na Al Ettifaq ya Saudi Arabia, lakini huenda akakaa nje kwa muda kutokana na kukosa vibali vya kazi.
Henderson aliyeondoka Liverpool dirisha lililopita la majira ya kiangazi baada ya kuwekewa ofa nono ya zaidi ya Pauni 700,000 kwa wiki amerejea Ulaya kwa kinachoelezwa hakuwa na furaha Saudia.
Hata hivyo, staa huyu atatakiwa kusubiri kwa muda hadi pale atakapopata kibali cha kazi kwa sababu Uingereza haipo kwenye Umoja wa Ulaya, hivyo hawezi kufanya kazi bila kibali.
Kiungo huyo ametua Ajax ingawa mchakato wake unaweza ukarahisishwa zaidi lakini kwa mujibu wa The Sun, huenda akasubiri kwa zaidi ya wiki mbili hadi kupata kibali, hivyo anaweza kuonekana uwanjani kuanzia Febuari.
Staa huyu mwenye umri wa miaka 33, ametua Ajax katika kipindi ambacho timu hiyo imerudisha makali yake baada ya kuwa na mwanzo mbaya wa msimu.
Kufungwa kwenye mechi tano kati ya tisa mwanzo kuliifanya kuwa kwenye nafasi za chini hadi kufikia Oktoba mwaka jana chini ya Kocha Maurice Steijn ambaye alifukuzwa na nafasi yake kuchukuliwa na kocha wa muda Van t’Schip, aliyewaongoza kushinda mechi sita kati ya nane za mwisho.