Pamoja na kuwa katika nafasi ya nne kutoka mwisho kwenye Ligi Kuu, Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Mecky Maxime amesema kutokana na maandalizi waliyonayo kwa sasa anaiona timu hiyo ikimaliza msimu ndani ya nafasi nne za juu na kucheza kimataifa.

Ihefu FC ipo jijini Arusha ilipoweka kambi ya muda kujiandaa na muendelezo wa ligi hiyo pamoja na Kombe la Shirikisho Tanzania bara ‘ASFC’ ambapo inatarajia kurejea Mbarali mapema mwezi Februari.

Timu hiyo kwa sasa ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi 13 ambapo ilianza msimu chini ya kocha John Simkoko kisha kumuachia majukumu Zuberi Katwila aliyerejea Mtibwa Sugar, na sasa mzigo upo kwa Maxime.

Akizungumzia maandalizi yao, kocha Maxime amesema anafurahishwa na ubora wa nyota wake akieleza kuwa maandalizi wanayoendelea nayo jijini Arusha timu hiyo itatisha.

Amesema pamoja na kutoanza vyema msimu, lakini matumaini yake ni kumaliza ligi ndani ya ‘Top 4’ ili kucheza michuano ya kimataifa iwe kupitia Ligi Kuu au Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

“Mawazo yetu ni kimataifa, vijana wanaendelea vyema na wanaonyesha matumaini makubwa. Binafsi naendelea kuitengeneza timu ili ligi inaporejea tufanye kweli,” amesema kocha huyo.

Nahodha wa timu hiyo, Joseph Mahundi amesema mapumziko waliyonayo yatawasaidia kurekebisha makosa yaliyojitokeza kuhakikisha wanaporudi uwanjani Ihefu inafanya kweli.

“Hatukuwa na mwanzo mzuri lakini kutokana na mapumziko haya na maboresho yaliyofanyika tunaenda kubadilisha upepo wa matokeo.” amesema nyota huyo.

Usajili waibua vita Young Africans
Baba mwenye Nyumba hasusii Mboga - Dkt. Nchimbi