Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la G77 na China, umeazimia kwamba nchi hizo pamoja na China zitaendelea kuweka utaratibu wa kuwakutanisha wataalamu wao kupitia wizara mbalimbali hususan katika maeneo ambayo wameyaainisha ili kuhakikisha hakuna nchi itakayoachwa nyuma kwenye mabadiliko ya sasa ya sayansi na teknolojia duniani.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipomwakilisha Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la G77 na China uliofanyika katika ukumbi wa Rwenzori Speke Resort Munyonyo jijini Kampala nchini Uganda. Mkutano huo ulianza Januari 21, 2024 na kuhitimisha Januari 22, 2024.
Amesema kikao hiko pia kimezungumzia maendeleo ya nchi wanachama katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kijamii, ulinzi na usalama pamoja na mwenendo wa uwekezaji kwenye mataifa hayo na kuona namna ambavyo wanaweza kujiimarisha wenyewe.
Akitoa kauli ya Tanzania katika mkutano huo, Majaliwa alisema nchi inaunga mkono mipango yote iliyoratibiwa na wataalamu kutoka nchi zinazounda umoja huo wakiwemo wa kutoka Tanzania kuhakikisha kwamba Taifa linakuwa sehemu ya mafanikio kulingana na mipango iliyopo kwenye nchi hizo zinazounda kundi la G 77 na China.
Amesema, “upande wa kisiasa tutaendelea kuimarisha mahusiano yetu ya kidiplomasia ambayo Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuanzishia na anaendelea nayo vizuri kuhakikisha tunaendelea kuwa na mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbalimbali. Vilevile kwenye sekta ya uchumi kama ambavyo Taifa letu limeendelea kuimarisha uchumi wa ndani kwa kutumia fursa tulizonazo kwa kushirikisha marafiki wanaoweza kutuletea mitaji.”
Katika Mkutano huo, Rais wa Uganda Yowezi Kaguta Museveni alikabidhiwa uenyekiti wa kundi hilo la G77 na China kutoka kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Cuba Salvador Antonio Valdés Mesa, ambapo alisisitiza ushirikiano kwa nchi hizo katika kushughulikia changamoto za kidunia na kutoa wito kwa mataifa yanayoendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo za nchi zinazoendelea.