Hakika yapo mambo ambayo wakati mwingine ukiyatafakari unaweza usiamini ukweli wake na kutaka uthibitisho zaidi, lakini uhalisia hubaki kuwa ndivyo ilivyo, kiasi ambacho Watu wengine huenda mbali zaidi kimawazo na kudhani kwamba ushirikina unahusika au wengine wakamtukuza MUNGU.
Nimeanza kwa aya hiyo, kutokana na aina ya ujumbe wa leo katika makala yetu unaohusu ‘Vifo vya aibu’ ambavyo viliwahi kuwakumba Wafalme waliopewa heshima katika nchi zao na majirani, lakini labda tujiulize aibu ni nini? Aibu ni hali ya kutokea kwa kinamasi, au kama mlivyozoea kwa neno rahisi kwamba ni fedheha.
Sasa wewe binafsi unaweza kujiuliza je, kifo gani ni cha aibu zaidi? maana Mtu anapotutoka ghafla huwa tunachukulia bahati mbaya, achilia mbali, kukutwa umekufa kwenye kitanzi yaani kujinyonga, hapo huwa tunasema huyu aliamua au alidhamiria kujiuwa kisha tunampumzisha na kuanza kuhoji kulikoni na wengine wakitoa lawama ama kwa Marehemu au Familia.
Wengine hudhani kwamba kufa kishujaa ni kufia vitani, au kufa ukiwa unahangaikia maisha na kutafuta riziki, au wengine hufikiria kwamba kufa baada ya kuugua kwa muda mrefu ndiyo kufa kishujaa au mtu akisafirishwa nje ya nchi kwa matibabu na akafariki basi huoan kwamba hicho ni kifo halali, lakini kwa nayekufa ghafla minong’ono huwa ni mingi na hata sababu hujengwa, yote ni mitizamo tu.
Duniani vipo vifo ambavyo viliwahi kuwa ni mjadala na vikaacha historia vikitafsirika kama vifo vya aibu kutokana na mazingira yake, ikiwemo kile cha Mfalme wa kwanza wa Uingereza, Mfalme Edmund kilichotokea mwaka 1016, kifo hiki kiliacha tafakuri jadidi na kukosekana kwa muafaka kuwa lipi ni jibu sahihi.
Hiki kilichukuliwa kama ni kifo cha aibu katika jamii, kwani Mfalme huyu aliuawa kwa kuchomwa kisu alipokuwa akifanya biashara zake na hivyo kuacha gumzo kwamba ni vipi Mfalme afe kwa kufanya biashara na ilikuwaje na wapi walikuwepo walinzi wake? ni aibu kwani mfalme ni mtu wa kuhudumiwa leo alikuwa na biashara ipi ya kumfanya mpaka achomwe kisu? watu walihoji.
Soma Makala hii kamili kwa kutembelea Website yetu ya Dar24 Media.
Wakati hilo likiacha historia, mwaka 1216, (miaka 200 baadaye), Umma wa waingereza pia uliarifiwa kwamba Mfalme Joh alikufa kwa ugonjwa wa kuhara, ilikuwa ni ajabu na watu walijiuliza sana inakuwaje mfalme aondoke kihivyo, kila mtu alisema lake lakini jibu sahihi lilikosekana, hilo nalo likaingia katika kumbukumbu na kuwaacha watu midomo wazi.
Haikuishia hapo kwani mwaka wa 1760, Mfalme George II pia akafariki. Inadaiwa alienda kwa mtengenezaji wake wa kiti cha enzi Porcelain, akiwa huko alizidiwa na Dkt. Frank Nicholls alisema Mfalme alikufa baada ya ateri ya kusambaza damu ya oksijeni katika mfumo wa mzunguko kupasuka, hapo napo maswali yakatokea eti ilipasukaje wakati Mfalme ana watabibu maalum je, hawakugundua mapema?.
Jambo likazua jambo, kikatokea kifo kingine tena cha Mfalme Henry wa Kwanza ambaye alikufa mwaka 1135 baada ya kula Samaki aina ya Taa. Inadaiwa kuwa Mfalme alipata shida kidogo ya choo na hivyo kupelekea mshituko wa tumbo na kuanza kuhara na baadaye kupoteza maisha.
Umma ukaibuka tena ukiona ni fedheha kwa Mfalme kufa kwa ugonjwa ambao hata uraiani unaweza kudhibitiwa, walidai kuna watumishi, kuna madaktari na pia wapo wasaidizi wake nini kilipelekea Mfalme afe kwa mchafuko wa Tumbo, walisema ni ajabu na nifedheha kwa Taifa hivyo wakakosa la kuamua zaidi ya kumuombea apumzike kwa amani.
Mfano leo hii eti tunasikia Kiongozi wa Nchi au Rais wa Taifa fulani amega Dunia kwa kula chakula kisha akaumwa tumbo, je kwa utandawazi huu unadhani itakuwaje, watafuta kiki wataandikaje, akina blog bin mitandao ya kijamii watatuambiaje? wapo pia ambao wataweka Vichwa vya Habari kwamba “Ukweli wote kuhusu kifo cha Kiongozi huu hapa,” yaani utadhani ni wao walimpakulia chakula.
Kiuhalisia matukio kama haya yanarandana na msemo ule waliwahi kuusema wahenga na hata wakati fulani Kundi la muziki wa Dansi la Twanga Pepeta katika kibao chao cha Mtu pesa, Marehemu Ramadhani Masanja (Banza Stone), kupitia moja ya ghani zake alisema “Shoka moja Mbuyu chini,” na hii imejidhihirisha wazi kwa wafalme hawa.