Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amesema asilimia 43 ya gesijoto, inahitaji kupunguzwa ifikapo mwaka 2030, ili kuwezesha joto la dunia kutoongezeka zaidi ya nyuzi joto 1.5.
Dkt. Jafo amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma.
Amesema, hatua hiyo itafanyika kwa kuongeza matumizi ya nishati jadidifu, kuongeza jitihada za kuachana na matumizi ya nishati chafuzi na kuondoa ruzuku kwa matumizi ya makaa ya mawe; kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na ushirikishwaji wa sekta binafsi na asasi za kiraia.
Aidha, amesema kuhusu mikakati ya kupunguza gesijoto, viongozi wa nchi wanachama walijadili jinsi ya kuimarisha jitihada za kupunguza uzalishaji wake hadi kubakia chini ya nyuzi joto 2.
Waziri Jafo amesema pia, majadiliano hayo yalihusu uanzishwaji wa programu ya upunguzaji wa gesijoto na haja ya kuondoa ufadhili na matumizi ya vyanzo vya nishati ya mafuta na makaa ya mawe kutokana na sababu za kuchangia katika uzalishaji wa gesijoto na uchafuzi wa mazingira duniani ambayo hata hivyo, makubaliano hayakufikiwa.