Kipyenga kimelia Msimbazi na mastaa wote wa Simba SC ambao hawashiriki Fainali za Mataifa ya Bara la Afrika ‘AFCON 2023’ wanatakiwa kufika leo Jumatano (Januari 24) na wawe tayari kambini kwa ajili ya kuanza mazoezi ya kujiandaa na mechi zijazo huku wenyewe wakitamba kwa kusema “Raundi hii tutaelewana.”
Hiyo ni baada ya kumalizika kwa siku 10 za mapumziko mafupi ambayo benchi la ufundi chini ya kocha Mualgeria Abdelhak Benchikha lilitoa kwa mastaa hao ili kupoza miili kutokana na Ligi Kuu kusimama kwa ajili ua kupisha fainali za AFCON 2023 zinaoendelea nchini Ivory Coast.
Hata hivyo, Simba SC haikutaka wachezaji wake wakae kizembe kwenye mapumziko hayo ndipo ikampa kila mmoja programu maalumu ya mazoezi atakayokuwa anafanya akiwa nyumbani kwake na pale atakaporejea kambini atakaguliwa kuwa aliitimiza kiufasaha.
Staa wa Simba SC, Willy Onana aliyemalizia mapumziko nchini kwao Cameroon alisema mapumziko waliyoyapata yamewasaidia kwenye kujitafakari na kujua nini wanatakiwa kufanya watakaporejea uwanjani
“Tumetumia muda huu kujitafakari wapi tulikosea na wapi tunatakiwa kuongeza nguvu pia kuweka mipango mipya, muda si mrefu tutarudi uwanjani, najua tutakuwa na ari mpya ya kupambana zaidi lengo ikiwa ni kuipa timu mafanikio,” amesema Onana ambaye ameonesha umahiri mkubwa tangu kocha Benchikha amechukua timu.
Kocha wa makipa wa Simba SC, Dani Cadena aliyemalizia mapumziko nchini kwao Hispania amesema kuwa, “Raundi hii tutaelewana. Kuna wachezaji wameongezwa na waliokuwepo wamepata muda wa kupumzika nadhani tukirejea kwa pamoja tutakuwa na nguvu kubwa na mashabiki wataifurahia timu yao,” amesema Cadena mwenye leseni ya ukocha ya UEFA pro.
Simba SC ina wachezaji 13 wa kigeni ambapo ukiwatoa Henock Inonga (DR Congo), na Clatous Chama (Zambia), walio katika Fainali za AFCON 2023, wengine wote walirejea makwao na sasa ni muda wa kurudi nchini tayari kuitumikia klabu hiyo.
Ayoub Lakred (Morocco), Che Malone Fondoh na Onana (Cameroon), Fabrice Ngoma (DR Congo), Sadio Kanoute (Mali), Saidi Ntibanzokiza (Burundi) na Aubin Kramo (Ivory Coast), wengi wao walienda kwao mapumziko na kuanzia Jana wameanza kurejea nchini sambamba na wale mastaa wapya watatu wa kigeni, Babacar Sarr anayetokea Senegal, Freddy Michael Kouablan kutoka Ivory Coast na Mgambia Pa Omar Jobe wote kufika leo Jumatano (Januari 24) majira ya jioni watakuwa kwenye kambi za Simba SC tayari kwa kuanza mazoezi kesho Alhamis (Januari 25).
Sio hao tu, pia maofisa wa benchi la ufundi wakiongozwa na Benchikha na msaidizi wake Farid Zemiti pamoja na kocha wa viungo Kamal Boujdjenane waliokuwa kwao Algeria, Cadena kutoka Hispania, Mtathimini michezo kwa njia ya Video ‘Video Analyst Mzimbabwe Kelvin Mavunga, na wengine wote waliokuwa makwao wamerejea jijini Dar es salaam.
Simba SC baada ya mapumziko hayo, itatupa karata yake ya kwanza kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, Februari 17 mwaka huu dhidi ya Dodoma Jiji, kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.