Kocha wa viungo wa timu ya Al Nasr ya Saudi Arabia, Junior Robertinho ambaye ni mtoto wa aliyekuwa kocha wa Simba SC, Robert Oliviera ‘Robertinho’ amesema kiungo mpya wa Msimbazi, Babacar Sarr ni mtu wa kazi.
Sarr aliyesajiliwa msimu huu kutoka US Monastir tayari amecheza mechi mbili, kwani aliposajiliwa tu aliikuta timu ikiwania ubingwa wa Kombe la Mapinduzi Zanzibar.
Japokuwa Wekundu hao hawakutwaa kombe hilo mbele ya mabingwa watetezi Mlandege, Sarr ni miongoni mwa wachezaji walioingia kipindi cha pili walipocheza dhidi ya Singida Fountain Gate, na katika mchezo wa fainali kocha alimpanga kikosi cha kwanza ingawa mitandaoni mashabiki hawakumuelewa.
Akizungumza na kwa njia ya simu kutoa Saudi Arabia, kocha Junior amesema amewahi kumuona kiungo huyo kwa muda wa dakika 90 walipocheza na US Monastir na alikuwa mchezaji hatari.
Ameeleza kuwa, hakuna mchezaji ambaye hana matokeo kwenye timu halafu akachezeshwa mechi nzima na hiyo tu inaonyesha ni aina gani ya mchezaji Simba SC wamempata.
“Niliwasikia makocha wake wakisema ni mchezaji mwenye nidhamu ya ukabaji na tulipocheza nao alikuwa na utulivu mkubwa uwanjani na kupokonya mipira kwa haraka hasa kwenye kufungua njia za kupitisha mipira,” amesema.
Ameongeza kuwa kiipaji chake kinaweza kuisaidia Simba ambayo imewahi kunolewa na baba yake aambaye alihitaji mtu mwenye uwezo wa kurudisha ugumu kwa timu pinzani.
Amesema: “Baba yangu alikuwa ananiambia Tanzania soka lao linatumia nguvu sana.
Pengine hilo ndilo eneo ambalo Sarr anatakiwa ajipange nalo, kwani timu aliyotoka alikuwa ni kiungo mstaarabu hakuwa na matumizi makubwa ya nguvu.”
Sarr anaonekana kuwa na kazi ya ziada ndani ya timu hiyo. kwani wachezaji anaocheza nao nafasi moja tayari walishaonyesha makali mbele ya kocha Abdelhak Benchikha na wanafahamiana namna ya uchezaji.
Viungo anaocheza nao ni Mzamiru Yasin, Fabrice Ngoma Sadio Kanoute na Abdallah Khamis.