Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Gambia Tom Saintfiet, ametangaza kujiuzulu baada ya timu ya nchi hiyo kutolewa katika hatua ya makundi ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ bila pointi yoyote.

Gambia ilipoteza mchezo wa mwisho wa Kundi C, kwa kufungwa mabao 3-2 dhidi ya Cameroon, na kuifanya nchi hiyo kuburuza mkia wa kundi, licha ya kuonesha kiwango safi kwenye michezo yote mitatu waliyocheza nchini Ivory Coast.

Saintfiet alijiunga na ‘The Scorpions’ kama Kocha Mkuu mwaka 2018 na kuiwezesha nchi hiyo kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka wa 2021 na 2023. Pia alifanikiwa kuipandisha Gambia katika viwango vya ubora wa Soka duniani, ambavyo hutolewa na ‘FIFA’ hadi nafasi ya 126 wanayoshikilia sasa.

Lakini Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji mwenye umri wa miaka 50 hakuona mafanikio hayo kuwa mazuri kiasi cha kumfanya abaki kama Kocha Mkuu wa timu ya taifa.

“Shukrani kwa Chama cha soka nchini Gambia na wafanyakazi wa Benchi la Ufundi. Nitaendelea kuwa shabiki wa Gambia milele. Binti yangu ana miaka 7, na nilipomwambia nitajiuzulu, hakufurahi. Lakini naamini huu ndio wakati mzuri kufanya hivyo,” amesema.

Hata hivyo Uongozi wa Chama cha Soka nchini Gambia umemshukuru Saintfiet kwa miaka mingi ya utumishi wake, na kubainisha kuwa “mtaalamu huyo” hatasahaulika nchini humo.

“Asante kwa huduma yako, Baada ya kila kitu kusemwa na kufanywa, Gambia hakika itakosa mbinu nzuri. Miaka mitano na nusu ya utumishi wa ajabu kwa taifa letu, na kutuwezesha kufuzu Fainali za AFCON mfululizo haikuwa bahati mbaya. Siku zote kila la heri,” imeeleza taarifa ya Chama cha soka nchini Gambia.

Juzi Jumatatu akiwa katika Mkutano na Waandishi wa Habari Kocha Saintfiet  alisema: “Hii ilikuwa mechi yangu ya mwisho kama Kocha wa Gambia. Mkataba wangu unaisha Agosti 2026, lakini nitaachia ngazi,” Mbelgiji huyo aliambia vyombo vya habari Jumatatu kufuatia kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Cameroon.

Atakayezembea kulipa kodi kutolewa - Ulega
Mtoto wa kike ni dira, alindwe - Majaliwa