Uongozi wa Chama cha Soka nchini Ghana ‘GFA’ umetangaza kusitisha Mkataba wa Kocha kutoka nchini England Chris Hughton, baada ya kushindwa kuivusha ‘Black Stars’ katika Hatua ya Makundi kwenda Hatua ya 16 Bora kwenye Fainali za AFCON 2023 zinazoendelea nchini Ivory Coast.

Uamuzi huo ulichukuliwa baada kikao cha dharura kilichowakutanisha Viongozi wa ‘GFA’, kufuatia kikosi cha Black Stars kutolewa kwenye Hatua ya Makundi bila kupata ushindi kwenye michezo mitatu ya Kundi B.

Taarifa ya GFA, iliyochapishwa na kusambazwa katika Mitandao ya Kijamii imeeleza kuwa, mbali na Kocha huyo kusitishiwa mkataba, pia Benchi la ufundi la Black Stars limevunjwa.

GFA imesema, katika siku zijazo, “itatoa ramani ya mustakabali wa Black Stars”

Hughton aliteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Black Stars Februari 2023, akichukua nafasi ya Otto Addo ambaye mkataba wake na timu ya taifa ya wanaume uliisha baada ya Fainali za Kombe la Dunia la 2022.

Hughton alipewa jukumu la kusimamia michezo iliyosalia ya Ghana ya kufuzu kwa AFCON 2023, kuipeleka Black Stars kwenye Fainali za ‘AFCON 2023’, na pia kusimamia kuanza kwa mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Dunia la 2026.

Kabla ya kuchukua wadhifa wa kocha mkuu, Hughton alitajwa kuwa Mshauri wa Kiufundi wa Black Stars, kabla ya mchujo wa mikondo miwili ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Nigeria, akisalia katika jukumu la mashindano ya Qatar.

Hughton ameitumikia Ghana katika mechi 13 akiwa kama Kocha Mkuu wa Black Stars, akiwa na rekodi ya kushinda mara nne, sare tano na kupoteza mara nne.

Katika mechi tisa za mashindano, kikosi cha Hughton kilipata ushindi mara tatu, kupoteza mbili na sare nne.

Kiwango cha uchezaji wa The Black Stars chini ya Kocha huyo wa zamani wa Brighton, Newcastle na Nottingham Forest umepata kuchunguzwa sana kama matokeo, na kuhitimisha kwa kusikitisha kwenye Fainali za AFCON 2023.

Uchaguzi wake na usimamizi wa michezo mara nyingi umekuwa ukitiliwa shaka na mashabiki na wachambuzi nchini Ghana.

Kufuatia kushindwa katika mechi ya ufunguzi na Cape Verde na kutoka sare na Misri na Msumbiji, Ghana ilitoka kwenye Fainali za AFCON 2023 kwa makala ya pili mfululizo kwenye hatua ya makundi.

Hughton alikubali kuwajibika kwa uchezaji mbaya nchini Ivory Coast.: “Ninawajibika kwa uchezaji huu na kukubali matokeo yangu na Black Stars hayajakuwa mazuri vya kutosha,” aliviambia vyombo vya habari baada ya sare ya 2-2 juzi Jumatatu na Msumbiji.

Black Stars italazimika kujipanga upya baada ya hali hiyo, huku tetesi za mechi mbili za kirafiki za kimataifa zikipangwa kufanyika Machi dhidi ya mabingwa wa dunia Argentina na China.

Kisha wataelekeza mawazo yao kwenye mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia zitakazorejea mwezi Juni, kwa mechi dhidi ya Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwakinyo: Nipo tayari kumchapa Mkongo
Salamu kutoka Saudi Arabia