Kocha Mkuu wa timu ya Soka ya Taifa ya Zambia, Avram Grant amesema hawaihofii Morocco kuelekea mchezo wa mwisho wa Kundi F wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika leo Jumatano (Januari 23).
Zambia ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kabla ya kupata sare nyingine kama hiyo dhidi ya Tanzania kwenye mchezo uliofuata ambapo walilazimika kusubiri mpaka dakika za mwisho kusawazisha kupitia kwa Mshambuliaji wake, Patson Daka anayechezea Leicester City.
Zambia inashika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo na watahitaji ushindi dhidi ya Morocco kuingia hatua ya 16 bora.
Morocco walipata ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Tanzania kabla ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya DRC.
Kwenye mchezo huo Simba hao wa Milima ya Atlas walitangulia kufunga kupitia kwa beki wa kulia wa Paris Saint-Germain, Achraf Hakimi kabla ya DRC kusawazisha baadae.
Kuelekea mchezo huo, Zambia itamkosa beki wake Roderick Kabwe aliyeoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Tanzania, huku Morocco wakikabiliwa na majeraha ya nyota wake lakini wanaweza kukifanyia marekebisho kikosi chake kwa kuwajumuisha Ayoub El Kaabi au Azzedine Ounahi.
Tunajua kuwa Morocco ni timu kubwa lakini hatuwaogopi. Tutacheza nao na nina imani tutaonesha kiwango kizuri. Tunatakiwa kuonyesha hali ya upambanaji,” amesema Grant.
“Kitu cha kwanza tunachotakiwa kufanya ni kusahau mechi zilizopita. Ni mashindano magumu kimwili na kiakili na kila mechi ina uhalisia wake,” amesema kocha wa Morocco, Walid Regragui.
Timu hizo zimekutana mara 18 huku Morocco wakishinda mara 10, Zambia mara sita na kutoka sare mara mbili.
Mechi ya karibuni kati ya timu hizo mbili ilikuwa ni kwenye Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani mwaka 2021 ambapo Morocco walishinda mabao 3-1.