Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Malale Hamsini amesema usajili wa Shiza Kichuya utairudisha timu yake nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza kocha huyo amesema uzoefu wa mchezaji huyo kwenye ligi pamoja na kucheza timu kubwa za Mtibwa Sugar, Simba SC na Namungo FC kutaongeza kitu kwao.
“Kichuya ni mchezaji mzoefu, lakini ameshapata mafanikio akiwa na Simba SC pia aliwahi kucheza soka la kulipwa nje hivyo vyote vitatuongezea kitu sisi, lakini pia wachezaji vijana watapata muda wa kujifunza kutoka kwake,” amesema Malale.
Kocha huyo amesema amepanga kumtumia mchezaji huyo katika eneo la pembeni lengo likiwa ni kutengeneza nafasi nyingi kwa washambuliaji wao.
Amesema mechi zilizopita walikuwa na upungufu mkubwa wa winga hivyo ujio wa mkongwe huyo umewasaidia kuwa na nafasi pana ya kubadili mifumo ya kucheza kulingana na mpinzani.
JKT Tanzania ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikikusanya pointi 16 katika michezo 14 iliyocheza hadi sasa.