Dereva Bodaboda, Amedius Mfoi (25), mkazi wa Muriet Jijini Arusha anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake, Amani Amedius Mfoi (3) Mkazi wa Morombo Mkoani humo.
Tarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Justine Masejo imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 23, 2024 muda wa saa 12:00 jioni katika mtaa wa Murieti Tarafa ya Elerai katika manisipaa ya jiji la Arusha.
Amesema mtuhumiwa huyo alimkata shingo mtoto huyo na kitu chenye ncha kali na kutenganisha kichwa na kiwiliwili, na baada ya taarifa hizo kufika Jeshi la Polisi walianza kumtafuta mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na wananchi na kumkamata muda mchache baadae.
Aidha, Kamanda Masejo amesema baada ya uchunguzi jalada litapelekwa ofisi ya taifa ya mashtaka kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.