Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi ameelezea kuridhishwa na viwango vinavyooneshwa na wachezaji wake wanaoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ wakiwa na timu taifa nchini Ivory Coast.
Young Africans imetoa wachezaji saba ambao wanatoka kwenye mataifa manne tofauti, mataifa hayo ni Tanzania, Zambia, Burkina Faso na Mali.
Wachezaji hao ni Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Mudathir Yahya na lbrahim Hamad Bacca’ (Tanzania), Djigui Diarra (Mali), Kenned Musonda (Zambia) na Stephene Aziz Ki (Burkina Faso).
Akizungumza Dar es salaam, Kocha huyo amesema amekuwa akifuatilia kwa makini michuano hiyo, hasa mechi ambazo kuna wachezaji wanaotokea kwenye kikosi cha Young Africans.
“Kikosi changu kimetoa wachezaji saba wengi wanaanza kwenye timu zao nimekuwa nafuatilia kwa makini na ukweli naridhishwa na viwango vyao na hata hao ambao hawapati nafasi ya kuanza siyo kwamba hawana uwezo, bali ni mapendekezo ya kocha,” amesema Gamnondi.
Kocha huyo amesema uwajibikaji wao wakiwa na timu zao za taifa unampa kazi nyepesi kuwaunganisha na wenzao ambao hawakuitwa kwenye timu za taifa kwa ajili ya michuano hiyo ya Afrika.
Amesema mpango wake ni kuwa na kikosi imara kitakachopambana na kufanya vizuri kwenye mashindano yote yajayo ikiwemo mechi mbili zilizobaki za hatua ya makundi za Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Kikosi cha Young Africans kinaendelea na mazoezi kambini kwao Avic Town, Kigamboni kikijiandaa na mechi za Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ambapo kwa sasa wanapigania kufuzu hatua ya Robo Fainali.