Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi ametoa michezo miwili kwa mshambuliaji wao mpya, Joseph Guede kwa ajili ya kuimarisha uwezo wake na kuongeza muunganiko na wachezaji wengine.

Guede ni miongoni mwa ingizo jipya ndani ya kikosi cha Young Africans amesajiliwa kipindi cha Dirisha Dogo ikiwa lengo la kuimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, akiwenmo Shekhan lbrahim na Augustine Okrah.

Mshambuliaji huyo ambaye alitarajiwa kutua nchini mwanzoni mwa juma hili lakini alikwamia Morocco kwa sababu ya visa, anatarajiwa kutua nchini leo Ijumaa (Januari 26) kujiunga na kikosi cha timu hiyo inayoendela na mazoezi Uwanja wa Avic Town, Kigamboni.

Gamondi amesema anahitaji kuimarisha kikosi chake na muunganiko pamoja na wachezaji wengine ndani ya kikosi hicho ambacho kinapambana kutetea taji lake la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Amesema anahitaji kupata muda wa kumwangalia nyota huyo ambaye amechelewa kuungana na wenzake kwa kumpa mechi na kutengeneza muunganiko na wenzake haraka kabla ya kurejea katika mashindano.

“Nahitaji kumwona Guede katika mechi itatulazimu kucheza michezo ya kirafiki katika kipindi ambacho tunasubiri ligi ianze, siyo yeye tu pia nataka kuona na maendeleo ya wachezaji wengine,” amesema.

Amesema Okrah na Shekhan walionekana katika Kombe la Mapinduzi na kufanikiwa kutengeneza muunganiko isipokuwa Guede ambaye bado hajafika.

Ameongeza kuwa, lengo la kuwa sawa wenzake ni kufikia malengo yao ambayo wamejiwekea ikiwemo kutwaa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.

Real Madrid kinara wa mapato duniani
Emilio Nsue: Nimefurahia kiwango AFCON 2023