Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa Tabora United ‘Nyuki wa Tabora’ Christina Mwagala amesema kwa usajili walioufanya kwenye dirisha dogo ni usajili wa maana na wenye faida kwa kuwa wanaamini wamesajili wachezaji wenye uwezo wa kuipambania timu hiyo na kuhakikisha malengo yanatimia.
Christina amesema kwamba, kila kitu kipo tayari ndani ya klabu kilichobakia ni ligi kuu kurejea na kisha wachezaji kuanza kuonyesha makali yao.
“Unajua kuna tofauti kati ya kuchukuwa wachezaji na kusajili wachezaji, sisi Tabora United tumesajili wachezaji tena wenye uwezo wa kushindana na timu yoyote ulimwenguni,
“Tumelitumia vizuri dirisha hili dogo tunakwenda kutimiza malengo yetu ya klabu mwisho wa msimu kutokana na wachezaji wetu tuliowasajili na malengo ya klabu ni kumaliza katika nafasi nne za juu na kama ikishindikana sana kwenye hizo nafasi basi nafasi ya tano itakuwa sahihi kwetu.
“Tumesajili wachezaji wazuri tena kwa kufuata ripoti ya kocha wetu mkuu Goran Kopunović. Kwa sasa timu yetu ipo Shinyanga kambini ambapo tuliamua kwenda kukita kambi huko kwa muda wa wiki mbili na tayari wiki ya kwanza imekamilika sasa tunakwenda kuianza wiki ya pili baada ya hapo tutatazama ratiba ya ligi inaelekeza vipi Ili tujue tunasalia Shinyanga au turudi nyumbani kuendelea namaandalizi ya ligi.”