Kocha Mkuu wa Liverpool Jurgen Klopp ameweka hadharani mpango wa kuondoka klabuni hapo, itakapofika mwishoni mwa msimu huu 2023/24.

Klopp, ametangaza uamuzi huo, huku ikibainika tayari ameshafanya kikao cha Uongozi wa Liverpool, na kuwaeleza kuhusu nia yake ya kuondoka klabuni hapo.

Klopp amethibitisha kufanyika kwa kikao hicho na ameahidi kuzungumza na wachezaji wake ili kuwaaga rasmi wakati bado wanaendelea kupambania matarajio yao msimu huu.

“Tulipokaa pamoja tukizungumza kuhusu wachezaji wanaoweza kusajiliwa, kambi ya majira ya joto ijayo na tunaweza kwenda popote, wazo likaja, ‘Sina hakika kuwa nipo hapa tena’ na nikajishangaa kwa hilo. Ni wazi naanza kufikiria juu ya hilo. ”

“Nitaondoka kwenye klabu mwishoni mwa msimu. Ninaelewa kuwa ni mshtuko.” Klopp amesema katika video yenye hisia kali iliyotumwa na Liverpool.

Klopp ameshinda mataji sita akiwa na Liverpool, likiwemo taji la Ligi Kuu ya England mwaka 2020 na kombe la Ligi ya Mabingwa mwaka mmoja kabla.

Liverpool kwa sasa ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England na kufika fainali ya Kombe la Carabao kati kati ya juma hili, wakati bado wapo kwenye Ligi ya Europa na Kombe la FA.

Aprili 2022, Klopp alisaini mkataba wa miaka miwili ambao ulitarajiwa kufikia kikomo mwaka 2026.

Kocha huyo kutoka nchini Ujerumani mwenye umri wa miaka 56 achukuwa nafasi ya Brendan Rodgers, Oktoba 2015, baada ya kujitengenezea heshima yake katika klabu ya Borussia Dortmund.

Akiwa Dortmund ilishinda mataji mfululizo ya Bundesliga mnamo 2011 na 2012 na akawapeleka hadi fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya mwaka 2013, ambapo walipoteza kwa Bayern Munich katika Uwanja wa Wembley.

Tanzania, Ivory Coast kusaini “MOU” sekta ya michezo
Ahmed Ally: Muda utafika na mtafurahi