Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kazi inayofanywa na taasisi za elimu ya juu ni kielelezo cha mchango wa sekta binafsi, katika kuchangia maendeleo ya Zanzibar kwa kuandaa wataalamu wa fani mbalimbali.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al -Sumait Chukwani, kilichopo Mkoa wa Mjini Magharibi na kuvitaka vyuo vikuu kuongeza programu zinazoakisi mahitaji ya nchi ikiwemo zinazohusu uchumi wa buluu.
Amesema, anapongeza juhudi zinazofanywa na Chuo hicho kinachomilikiwa na Shirika la Direct Aid ya Kuwait kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya elimu Zanzibar tangu kuanzishwa kwake 1998.
Rais Dkt. Mwinyi pia amevihimiza vyuo kujikita katika utafiti utakaotoa ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili jamii kwa kushirikiana na taasisi na idara mbalimbali za Serikali.
Mahafali hayo, yamehudhuriwa na Mkuu wa Chuo cha Abdulrahman Al-Sait, Rais Mstaafu Dkt Amani Abeid Karume , Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini na Vyombo vya ulinzi na usalama.