Baada ya kushinda mkanda wa WBO Afrika, bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo amesema siri ya ubingwa huo ni mbinu bora alizopewa na makocha wake.
Bondia huyo alishinda mkanda huo baada ya kumpiga Elvis Ahorgah raia wa Ghana kwa TKO katika raundi ya saba, pambano la uzito wa kati lililofanyika Uwanja wa Ndani wa Amaan Complex, Unguja.
Mwakinyo amesema makocha wake Kanda Kabongo na Amos Nkondo ‘Amoma’, ndiyo wanaostahili pongezi kutokana na kumpa mbinu bora wakati wa maandalizi.
Amesema ubora wa makocha hao ndiyo sababu kubwa ya kuonyesha kiwango kikubwa na kushinda mkanda huo mkubwa.
“Nashukuru timu yangu walisimama mimi hadi kushinda mkanda huu, ninawaamini makocha Kanda Kabongo na Amoma watanipeleka juu,” amesema
“Hii ni zawadi kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, nimeweka historia kubwa hapa nchini kushinda mkanda huu, pia nimeingia katika familia ya WBO,” amesema.
Naye Promota wa pambano hilo, Meja Selemani Semunyu, amesema baada ya kumalizika kwa pambano hilo, wadau wa masumbwi nchini watagemee burudani nyingine nzuri zaidi kutoka katika kampuni yake.
“Watu wanatamani kuwepo kwa pambano la Mwakinyo na Twaha Kassim ‘Kiduku’, muda ukifika watacheza japokuwa wote nimeshaongea nao na kusikiliza ofa zao,” amesema