Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Angel Gamóndi, amesema wanakwenda kucheza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Housing FC ya Njombe kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam, ili kujiweka sawa na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo ambaye yuko na kikosi hicho kwa wiki mbili sasa akikifua kuanzia kwenye ufukwe wa Coco na baadae uwanjani, amesema ni muhimu kushinda mechi hiyo kwa sababu ni moja kati ya makombe makubwa Tanzania, lakini itawafanya wachezaji wake kujiamini zaidi, hivyo atautumia mchezo huo kama mazoezi ili kupima kikosi chake kama kimesharejea kwenye mtiririko na kasi anayoitaka kwa ajili ya michuano mingine.

“Tunakwenda kucheza mechi ya FA, tunajiandaa kushinda mechi hii kwa sababu itaturejesha kwenye morali, pia hatutaki kulipoteza kombe hili, lakini ni mchezo ambao kila mchezaji anatakiwa aonyeshe kuwa amerudi kwenye kiwango chake kile cha mwanzo au zaidi kwa sababu ni kama mazoezi kuelekea Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema kocha huyo kutoka nchini Argentina.

Amesema hadhani kama wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa watacheza mechi hiyo kwa sababu watakuwa wamechelewa na watahitaji wapumzike, badala yake wachezaji atakaowatumia wengine wao ni wale alioanza nao mazoezi.

Young Africans itacheza mechi ya kwanza baada ya wiki tatu kupita tangu ilipotolewa kwenye hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika mjini Zanzibar na kushuhudia Mlandege ikitwaa tena ubingwa kwa mara ya pili, ikifunga Simba SC bao 1-0.

Itakuwa wiki tano tangu ilipocheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Desemba 23, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma dhidi ya Tabora United, ikishinda bao 1-0, ambapo kuanzia hapo haijacheza mechi yoyote Bara.

Tayari, wachezaji Maxi Nzengeli na Clement Mzize wameshatoa yao ya moyoni kuhusu kuwamisi mashabiki wa soka kutokana na kukaa muda mrefu bila kucheza.

Walisema wanawakumbuka mashabiki wa timu hiyo jinsi wanavyokuwa nao kila wanapokwenda na wanavyowashangilia kitu ambacho kinawapa moyo wa kupamba kwa ajili yao, hivyo wana hamu ya kuwaona tena.

Ratiba inaonyesha kuwa baada ya hapo, Young Africans inatarajiwa kushuka dimbani kwa mara ya kwanza katika mechi ya Ligi Kuu, Februari 16, kucheza dhidi ya JKT Tanzania.

Benchikha: Tupo tayari kumkabili Tembo
Kivumbi 2023/24 kuendelea tena Bara