Na Humphrey Edward.

Nchini Tanzania, kumekuwa na matukio au taarifa mbalimbali zikianisha uwepo wa tatizo la saratani ya shingo ya kizazi, ambayo husababishwa na aina ya kirusi kinachoitwa ‘Human Papilloma Virus’ HPV, ambacho huambukizwa kwa njia ya kujamiiana na mtu mwenye maambukizi.

Hali hii imekuwa ikisababisha idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo, na hata kupelekea baadhi ya Wanawake kukosa watoto kutokana na madhara ya ugonjwa huo hatari kwa avya ya akina mama na ugonjwa huu husababisha mateso makubwa, licha ya kuwa unaweza kuzuilika kabisa ikiwa itagunduliwa mapema, kwani ni moja ya saratani zinazoweza kutibika.

Shingo ya kizazi ni nini?

Shingo ya kizazi ‘cervix’ ni sehemu ya kizazi kati ya uke na mji wa mimba ambapo sehemu hii ina kazi nyingi ikiwemo kupitisha mbegu za kiume kuelekea katika mji wa uzazi na hatimaye mirija ya uzazi, ili kupevusha yai, kupitisha damu ya hedhi na ni mlango anaopitia mtoto wakati wa kuzaliwa.

Shingo hii ya kizazi, hupata maambukizi na kupelekea upataji wa saratani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo, kushiriki tendo ndoa katika umri mdogo au chini ya miaka 18, kuwa na wenzi tofauti au mwenzi aliye na wapenzi tofauti, utumiaji wa sigara ambao hupunguza nguvu ya kinga mwilini, kuwa na kinga hafifu ya mwili au magojwa kama Ukimwi na uzazi wa mara kwa mara.

Kutokana na hali hii, Dar24 ilimtafuta Daktari wa Magonjwa ya akina mama, Massine Mkwawa ambaye alisema aina hii ya Saratani ya shingo ya kizazi hutokana na mabadiliko ya mfumo wa chembechembe au seli zilizoko katika shingo ya kizazi, ambapo mabadiliko haya hupelekea chembe chembe hizo kushamiri na kuzaliana kwa kasi kinyume na mpangilio wa maumbile.

Anasema, “Wanawake wanaoishi na Virusi vya UKIMWI – VVU wana uwezekano mara sita zaidi wa kupata saratani ya shingo ya kizazi ikilinganishwa na idadi ya watu na inakadiriwa kuwa asilimia 5 ya visa vyote vya saratani ya mlango wa kizazi huchangiwa na VVU. VVU katika saratani ya shingo ya kizazi huathiri vibaya wanawake wenye umri mdogo na matokeo yake, asilimia 20 ya watoto wanaopoteza mama zao, hutokana na saratani ya shingo ya kizazi.”

Inasemekana kuwa, Saratani ya shingo ya kizazi inaongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake katika nchi zinazoendelea na ripoti ya mwaka 2012 ya shirika la afya duniani (WHO), ilieleza kuwa kati ya matukio 75,000 ya waathirika wa saratani ya kizazi barani Afrika, 50,000 walifariki dunia.

Aidha, takriban asilimia 90 ya vifo 342,000 vilivyosababishwa na saratani ya shingo ya kizazi hutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, huku viwango vya juu zaidi vya saratani hiyo na vifo hutokea katika bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, Amerika ya Kati na Kusini Mashariki mwa Asia.

Ni wazi kuwa kutokana na hali hii ndipo Shirika hilo WHO, likaamua kuitangaza Januari kuwa ni mwezi wa kuhamasisha jamii kuhusu saratani ya shingo ya kizazi, likibainisha kuwa ulimwenguni kote, saratani hiyo ni ya nne kwa Wanawake ambao walikuwa ni wagonjwa wapya 604,000 wa mwaka 2020.

Sababu za Ugonjwa.

Kwa mujibu wa takwimu za kitaalamu ambazo pia zimetolewa katika Hospitali Rufaa ya Ligula iliyopo Mkoani Mtwara, inaeleza kuwa ripoti ya utafiti wa kisayansi zimeafiki kuwa asilimia 99 ya saratani za shingo ya kizazi hutokana na maambukizi ya virusi vya ‘Human Papillomavirus’ au HPV, vilivyoko katika jamii ya papilloma.

Baadhi ya virusi hivi vyenye aina zaidi ya mia moja huambukizwa kwa njia ya kujamiana na ni maambukizi ya kawaida ya zinaa ambayo yanaweza kuathiri ngozi, sehemu za siri na koo na takriban watu wote wanaofanya ngono wataambukizwa wakati fulani wa maisha yao, kwa kawaida bila dalili.

Hata hivyo, Dkt. Mkwawa yeye anasema mara nyingi mfumo wa kinga huondoa (HPV) kutoka katika mwili na maambukizi ya mara kwa mara ya HPV yanaweza kusababisha seli zisizo za kawaida kukua, ambazo huendelea na kuwa saratani, aidha, maambukizi ya mara kwa mara ya HPV kwenye shingo ya kizazi ikiwa haitatibiwa, husababisha asilimia 95 ya saratani ya mlango wa kizazi.

“Na kwa kawaida, inachukua miaka 15-20 kwa seli zisizo za kawaida kuwa saratani, lakini kwa wanawake walio na kinga dhaifu, kama vile wenye VVU isiyotibiwa, lakini kwa wanawake walio na kinga dhaifu, kama vile wale wenye VVU isiyotibiwa, mchakato wa ugonjwa huu unaweza kukuwa haraka na kuchukua miaka 5-10,” alifafanua Dkt. Mkwawa.

Dalili.

Ugonjwa huu wa Kansa ya shingo ya kizazi huanza na kuendelea kwa muda mrefu bila kuonesha dalili zozote, ambazo zinaweza kujitokeza wakati ugonjwa upo katika hatua za mwisho kwa kutokwa na damu isiyo ya hedhi, kutokwa na damu ukeni baada ya kujamiiana na kutokwa na damu ukeni kwa wanawake waliokwisha kukoma hedhi.

Dalili nyingine ni Damu iliyochanganyikana na majimaji ya uke, matone ya damu au damu kutoka kipindi kisicho cha hedhi, kutokwa na majimaji au uchafu ukeni wenye harufu mbaya wakati mwingine ukiwa umechanganyika na damu, maumivu wakati wa kujamiiana, maumivu chini ya tumbo, nyonga na kiunoni, kukojoa mkojo wenye damu na upungufu wa damu.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, – WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema kwa takwimu za mwaka 2020 pekee, ni asilimia 13 tu ya watoto wa kike wenye umri wa miaka 9 hadi 14 duniani walipewa chanjo dhidi ya virusi vinayovabisha saratani hiyo, au HPV.

Anasema, Wanawake na wasichana katika nchi masikini ndio wanakosa fursa za kupata vituo vya kwenda kupimwa virusi hivyo, chanjo ya HPV na matibabu huku katika miaka 11 iliyopita, watengenezaji wameelekeza nguvu ya usambazaji wa chanjo ya kupambana na ugonjwa huo katika maeneo tajiri zaidi.

Dkt. Tedros anaongeza kuwa, “ndio maana takriban nchi 80 ambazo ndio zina jumla ya theluthi mbili ya mzigo wa saratani ya shingo ya kizazi duniani bado hazijaanzisha chanjo hii ya kuokoa maisha ya Wanawake. Ni ama ilivyo katika janga la Uviko-19 pengo katika kiwango cha vifo ni dhahiri vifo 9 kati ya 10 vinatokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati.”

Tiba.

Matibabu ya saratani hutolewa kulingana na hatua ya ugonjwa, ambapo ugonjwa ukiwa hatua za mwanzo huweza kutibika kabisa (ingawa kuna uwezekano wa kujirudia), vilevile hatua za mwisho za ugonjwa huu huwa haziwezi kumponya mgonjwa kabisa na kinachofanyika mara nyingi ni kutoa matibabu yatayotuliza dalili na maumivu na kumuwezesha mgonjwa kuishi vizuri.

Huduma za matibabu hutolewa kwa njia za upasuaji katika hatua za mwanzo za ugonjwa, Mionzi, Dawa za Saratani na Mionzi pamoja, hivyo kukuza ufahamu kwa kutoa elimu kwa jamii, husaidia kuzuia na kudhibiti katika kipindi cha maisha yote ya Mama. Kupata chanjo katika umri wa miaka 9-14 pia ni njia nzuri ya kuzuia maambukizi ya HPV, saratani ya mlango wa kizazi na saratani zingine zinazohusiana na HPV.

Baadhi ya waathiriwa wa Ugonjwa huu akiwemo Joyce Mzengo anasema mbinu hizi zilimsaidia kupata ahueni na hata mtoto wake mkubwa alipougua aliweza kurejea hatika hali yake ya kawaida kwa kuwahi kupata huduma bada ya kugunduliwa mapema na kufuata matibabu ya haraka yaliyoweza kumtibu saratani ya shingo ya kizazi.

“Kuna kitu kinaitwa Pap test kinafanyika mara 1 kwa mwaka au mara 1 kwa miaka 2- 3, lakini itategemea ushauri wa daktari, umri wako, hali ya afya na majibu mtu aliyoyapata katika chunguzi za awali na mfumo wa maisha, na hata alipowahi mwenyewe alimshukuru MUNGU akisema hatoweza kupuuza tena uchunguzi wa afya lakini hii ilisaidia kwakuwa mimi nialianza,” amasema Bi. Joyce.

Chanjo.

Inaarifiwa kuwa, hadi kufikia mwaka 2023 kuna chanjo 6 za HPV zinazopatikana ulimwenguni zote zikilenga kulinda aina hatarishi za HPV 16 na 18, ambazo husababisha saratani nyingi za mlango wa kizazi na zimeoneshwa kuwa ni salama na zenye ufanisi katika kuzuia maambukizi ya HPV na saratani ya shingo ya kizazi.

Wataalamu wa masuala ya Afya, wanasema chancho hizi zinapaswa kutolewa kwa wasichana wote wenye umri wa miaka 9-14, wa umri wa kubalehe na kabla ya kuanza kujamiiana na zinaweza kutolewa kama dozi 1 au 2.

Kwa walio na kinga iliyopunguzwa wanapaswa kupokea dozi 2 au 3 lakini baadhi ya nchi pia zimeanza kuwachanja wavulana, ili kupunguza zaidi maambukizi ya HPV katika jamii na kuzuia saratani kwa wanaume zinazosababishwa na HPV.

Hata hivyo, kuna njia nyingine ya kuzuia maambukizi ya HPV ambayo ni kutovuta au kuacha Sigara, kutumia kondomu, kutahiriwa kwa wanaume kwa hiari nk.

Hitimisho.

Julai 23, 2023 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema akina mama 1,300 waliokuwa na Saratani ya Mlango wa kizazi na ambao walianza kupatiwa matibabu katika Taasisi ya Ocean Road ya Jijini Dar Es Salaam, 98 kati yao walipona na kuruhusiwa kurejea majumbani mwao.

Majaliwa alisema Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kuhakikisha kunakuwa na ustawi wa afya ya mama na mtoto ikiwemo mpango wa Mama Samia Mentorship Program na kuongeza wigo wa kutoa huduma za kupima dalili za awali za saratani ya uzazi kutoka Vituo vya Afya 925 vilivyopo, hadi kufikia vituo vya Afya 1,025.

Siku hiyo, kauli ya Waziri Mkuu ilitanguliwa na ile ya Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu ambaye alisema, “kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2021 mpaka sasa takribani wanawake 40,000 walifikiwa na huduma ya mkoba ambazo zinajumuisha huduma za elimu, uchunguzi wa awali, rufaa na matibabu ya saratani kupitia programu maalumu inayojulikana kama ‘Samia Suluhu Hassan Outreach Program’.”

Prof. Nagu pia aliwarai Watanzania kuzingatia mtindo Bora wa Maisha ili kujikinga na Magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya saratani na kuwaasa wanawake kupima saratani ya mlango wa kizazi kwani endapo itagundulika mapema, Saratani ya Mlango wa Kizazi inatibika na kupona.

Pamoja na maelezo hayo ya matumaini, bado Wanawake wanapaswa kuchunguzwa saratani ya shingo ya kizazi kila baada ya miaka 5-10 kuanzia umri wa miaka 30 na kwa Wanawake wanaoishi na VVU, wao wanapaswa kuchunguzwa kila baada ya miaka 3 kuanzia umri wa miaka 25 ili kupata majibu sahihi na njia za kufuata.

Ikumbukwe kuwa, Mkakati wa kimataifa unahimiza angalau kufanya uchunguzi mara mbili kipimo cha juu cha HPV katika umri wa miaka 35 na tena katika miaka 45, kwani ugonjwa wa saratani ni mara chache huwa unatoa dalili, na ndiyo maana uchunguzi wa mara kwa mara wa saratani ya shingo ya kizazi ni muhimu, hata kama umepata chanjo ya dhidi ya HPV.

NBS kuzalisha takwimu bora kwa njia rafiki
Watakaochangia mfuko wa Elimu kunufaika - Dkt. Kipesha