Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Francis Baraza amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara 2023/24.
Akizungumza kocha huyo kutoka nchini Kenya amesema wamefanya maandalizi ya kutosha wakati wa mapumziko ya ligi hiyo kupisha michuano ya Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ inayoendelea nchini Ivory Coast.
“Tupo tayari kwa vita ya pointi tatu, tumepata muda wakutosha kurekebisha mapungufu yetu lakini pia tumecheza mechi kadhaa za kirafiki ambazo zimetuimarisha na kujiona tupo tayari kwa kazi,” amesema Baraza.
Kocha huyo ambaye amewahi kuzitumikia Kagera Sugar na Biashara United, amesema anajua wanakabiliwa na michezo migumu ukiwemo dhidi ya Simba SC, lakini wamejipanga kuhakikisha wanachukua pointi zote tatu kwenye mchezo huo.
Amesema kila mchezaji ana ari kubwa yakuonesha kile alichokuwa nacho na kuipigania timu yake.
Dodoma Jiji ipo nafasi ya saba kwenye msimamo ikikusanya pointi 18 katika michezo 13 waliyocheza hadi sasa.