Kocha Mkuu wa Namungo FC Mwinyi Zahera, amewataka wachezaji wake kutokamia mechi kubwa tu inapocheza na Klabu za Simba SC, Young Africans au Azam FC halafu mechi zingine wanacheza kivivu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam ambako kikosi hicho kimepiga kambi, Zahera amesema kama wakipambana vizuri kwa kila mechi kucheza kama iliyopita bila kuangalia wanacheza na timu gani, basi ana uhakika kikosi chake kitafanya vizuri.
Zahera amechukua mikoba ya kukinoa kikosi hicho, baada ya kuondoka Cedric Kaze na baadae Denis Kitambi, huku mwenyewe akiwa ametokea Coastal Union kama mkurugenzi wa programu za vijana.
Tulianza mazoezi rasmi Januari 12, programu inaendelea, tunafanya mazoezi mara mbili, siku nyingine mara moja kutokana na mvua wakati mwingine, inasumbua kidogo.
Wachezaji wengi wamesharejea, kila kitu kipo sawa, na kama wachezaji wangu watapambana sawa kwa nguvu ile ile kila mechi basi tutamaliza ligi tukiwa sehemu nzuri sana, lakini tatizo la timu nyingi za Kitanzania ni kuzikamia timu kubwa za Simba SC, Young Africans na wakati mwingine Azam FC, wakicheza nazo wanapambana kweli kweli, ila baada ya hapo wanapocheza na timu zingine wanacheza kawaida tu utashangaa, wanachotakiwa ni kucheza hivyo kilamechi, nimewaambia wachezaji wangu waachane na hilo, badala yake kila mechi wacheze kama fainali,” amesema Zahera.
Namungo FC ipo nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuendelea mwishoni mwa juma hili hii baada ya kusimama kupisha Fainali za Mataifa ya Afrika, AFCON.
Timu hiyo ina pointi 17 kwa michezo 14 iliyocheza, ikishinda minne, sare tano na kupoteza mechi tano pia.