Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini – TPSF, imemteua Raphael Maganga kuwa Mkurugenzi Mkuu Mpya kuanzia Februari 1, 2024.
Taarifa iliyotolewa na Bodi hiyo hii leo Januari 30, 2024 imeeleza kuwa Maganga anachukua nafasi ya Balozi. John Ulanga, ambaye aliteuliwa kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Maganga ambaye alikuwa akiikaimu nafasi hiyo, anatazamiwa kuleta uzoefu na utaalamu katika maendeleo ya sekta binafsi, diplomasia ya uchumi na uwekezaji na biashara, kutokana na kufanya kwake kazi nchi kadhaa ikiwemo Australia, Kenya na China.
Kabla ya kujiunga na TPSF mwaka 2021 kama mshauri wa sekta binafsi, pia aliwahi kuwa mwakilishi wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) kwa Tanzania na Burundi, lililolenga kushughulikia mazingira ya biashara katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.