Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imeendelea kusimamia uwekaji wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA thabiti ya kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma za kisheria ikiwemo kupata elimu ya masuala ya sheria, ufunguaji wa kesi, uendeshaji wa kesi, upatikanaji wa nyaraka za kesi na ushahidi, hukumu na maamuzi ya kesi na uwepo wa vyombo vya utoaji haki katika ngazi za kijamii na upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria.
Waziri Chana ameyasema hayo hii leo Januari 30, 2024 Jijini Dodoma kwenye hafla ya ugawaji wa vifaa vya TEHAMA vilivyonunuliwa na Serikali ya awamu ya sita ambavyo ni Kompyuta, Seti za Video Conferencing, Printer na Vifaa vya Mtandao lengo ni kuziwezesha Taasisi za Haki Jinai kutoa huduma kwa wananchi kwa kutumia fursa za mifumo ya TEHAMA iliyojengwa.
Amesema, moja ya jukumu kubwa la Wizara, ni kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati bila kujali dini, umbali au hali yoyote ya mtu. Ili kufanikisha hilo, kwani Serikali inatambua umuhimu wa mifumo imara ya utoaji na upatikanaji wa haki; ambapo imetoa kipaumbele cha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwani matumizi ya Teknolojia yatawapunguzia wananchi muda na gharama za kushughulikia masuala ya kisheria na badala yake watajikita zaidi katika shughuli za kiuchumi na kimaendeleo.
Aidha, ameongeza kuwa Mahakama ya Tanzania imepatiwa Seti za kuendesha mashauri kwa njia ya Mtandao ambazo zitaharakisha uendeshaji wa mashauri na kupunguza mlundikano wa mashauri kwa Majaji na Mahakimu, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imepatiwa kompyuta ambazo zitarahisisha utendaji na matumizi wa mfumo wa kushughulikia majalada ya Mashtaka ili kupunguza mlundikano wa majalada ya upelelezi na kuongeza kasi ya upatikanaji wa haki jinai.
Gereza la Msalato na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe-Sehemu ya Isanga zimepatiwa vifaa vya TEHAMA vitakavyowezesha uendeshaji wa mashauri pamoja na matumizi ya huduma za kisheria kupitia mifumo iliyopo kwa lengo la kuleta maboresho na haki za wafungwa na mahabusi na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoani Njombe, Magereza ya Ludewa na Njombe Mjini yatafungwa vifaa hivyo vya kisasa ili kuwezesha na kurahisha uendeshaji wa mashauri pamoja na upatikanaji wa hukumu kwa wakati.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Mary G. Makondo amesema
Kuimarika kwa matumizi ya TEHAMA kunawezesha kuziunganisha taasisi za Haki Jinai katika mfumo mmoja wa kielektroniki katika kuwasiliana kiutendaji na hivyo kuimarisha ubora na upatikanaji wa huduma za kisheria zinazotolewa na Taasisi hizo.
Amesema, Wizara kupitia mradi huo imefunga miundombinu ya kuendesha mashauri kwa njia ya mtandao (Video Conferencing) katika Magereza sita (06) hapa nchini. Magereza haya ni Gereza la Isanga Dodoma, Gereza la Mkoa wa Singida, Gereza la Mpanda, Magereza ya Songea na Kitai Mkoani Ruvuma na Gereza la Kiteto Mkoani Manyara; Tume ya Kurebisha Sheria na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Songwe zimepatiwa Kompyuta kwa ajili ya kusaidia utendaji kazi.