Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Morocco Walid Regragui amekubali kubebe lawama za timu yake kutupwa nje ya Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ baada ya kubanjuliwa na Afrika Kusini usiku wa kuamkia leo Jumatano (Januari 31).
Morocco ‘Simba ya Atlas’, ambao walipewa nafasi kubwa ya kutwaa Ubingwa wa ‘AFCON 2023’, imetupwa nje katika fainali hizo kwenye Hatua ya 16 Bora kufuatia kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Afrika Kusini.
Evidence Makgopa aliifungia Afrika Kusini bao la kuongoza dakika ya 57 kabla ya Teboho Mokoena kufunga bao la pili na la ushindi kwa mkwaju wa faulo katika muda wa nyongeza.
Dakika chache kabla ya bao la ushindi la Mokoena, Achraf Hakimi kupata nafasi ya kufunga bao 1-1, lakini beki huyo wa Klabu BIngwa nchini Ufaransa PSG alikosa mkwaju wa Penati, jambo ambalo liliwasikitisha Mashabiki wa Timu ya Taifa ya Morocco.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Regragui alisema: “Tulifanya makosa mengi ya kiufundi na tulikosa uvumilivu katika mchezo wa kujiimarisha. Tulikuwa na haraka sana na tulikuwa na fursa chache.
“Mechi ingeweza kuamuliwa katika kipindi cha kwanza, lakini kwa kiwango hiki, kila nafasi iliyopotea inaadhibiwa mara moja.
“Tulijaribu mwishowe na tukapewa Penati, lakini tulikosa. Ingeweza kusawazisha bao na kuturudisha mchezoni, lakini kukosa Penati kulituumiza sana.
“Hakika hatukufanya yale tuliyotakiwa, na tulikosa baadhi ya vitu muhimu. Sina budi kubeba lawama zote za timu hii.
“Wachezaji walitoa kila kitu na kutekeleza maagizo yangu, tutajifunza kutokana na kushindwa kusikotarajiwa. Tulikuja kwa unyenyekevu mkubwa, lakini lazima tukubali kwamba tumeshindwa.
“Ni jambo la kusikitisha sana kwa mashabiki wetu ambao walituunga mkono kwenye mashindano, na walitusaidia sana, ninarudia ninapaswa kubebeshwa lawama zote.”