Kocha wa zamani wa Timu ya Taifa ya Misri Hassan Shehata amelitaka Shirikisho la Soka nchini humo ‘EFA’ kumtimua Kocha wa sasa Rui Vitoria na kumteua Hossam Hassan kama mbadala wake.
Shinikizo hilo la Shehata limekuja, kufuatia Timu ya Taifa ya Misri kutupwa nje ya Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ kwa kufungwa na DR Congo kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati usiku mwishoni mwa juma lililopita, nchini Ivory Coast.
Mafarao walifuzu kwa hatua ya mtoano baada ya sare ya 2-2 katika Kundi B dhidi ya Msumbiji, Ghana, na Cape Verde, kabla ya kuambulia sare nyingine dhidi ya DR Congo katika Hatua ya 16 Bora.
Kwa ujumla, vijana wa Rui Vitoria hawakuweza kushinda mchezo hata mmoja nchini Ivory Coast na wamerejea Misri wakiwa na sare nne, jambo ambalo lilitia shaka mustakabali wa kocha huyo.
Akimzungumzia Kocha huyo kutoka nchini Ureno, Shehata ambaye alifanikiwa kuiwezesha Misri kutwaa Ubingwa wa Afrika mara tatu amesema: “Vitoria haitakiwi kuendelea kukinoa kikosi cha Misri kwa sababu hajafanya lolote, katika masuala ya ukocha, hajawaendeleza mabeki. Lazima aondoke.
“Ninasema hivi si kwa sababu mimi ni kocha au ninatamani chochote. Misri ni moja ya nchi kubwa katika soka Barani Afrika, lakini pamoja naye, hatujaona chochote.
“Mbadala wa Vitoria lazima awe kocha wa kitaifa. Sio kwa sababu ninataka kuchukua jukumu, lakini lazima ulete kocha anayejua wachezaji wa nchi yake na anajua jinsi ya kukabiliana nao.
“Kocha yeyote wa Misri anaweza kuinoa timu ya taifa. Hossam Hassan ni jina kubwa sana.”