Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Burkina Faso, Hubert Velud, amesema itamlazimu kutafakari kichapo chao cha 2-1 dhidi ya Mali katika mchezo wa Hatua ya 16 Bora, kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ uliyochezwa jana Jumanne (Januari 30).
Bao la bahati mbaya la kujifunga la Edmond Tabsoba pamoja na Lassine Sinayoko kipindi cha pili lilitosha kwa Kikosi cha Mali kutoka kifua mbele kwenye Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly, Ivory Coast.
Mkwaju wa Penati wa Bertrand Traore ulionyesha faraja kwa waliofika fainali 2013 na Velud amekiri wamepoteza dhidi ya timu bora ambayo ina ubora, haswa katika safu ya kati.
“Kwa kweli sina wa kumlaumu. Tumepoteza dhidi ya timu bora. Mali wana wachezaji wazuri. Tulipata nafasi lakini pia tulianzisha wachezaji wapya. Sikushangazwa na ubora wa timu hii. Ubora mzuri sana na viungo wa kiwango cha juu.” amesema Velud
Kocha huyo amesema watapitia uchezaji wao kwa nia ya kupata chanzo cha kushindwa kwao dhidi ya Mali.
“Tutazingatia kushindwa huku. Tunapaswa kukagua na kuchambua mazuri na mabaya wakati wetu hapa,” amesema
Pia amesifu Fainali za AFCON za mwaka huu kama mojawapo ya michuano ya bara iliyopangwa vyema zaidi lakini akajivunia kuondoka katika shindano hilo linalofanyika kila baada ya miaka miwili kabla ya wakati wake.
“AFCON 2023 iko wazi kwa yeyote kushinda. Ni moja ya AFCON bora zaidi kwa upande wa mpira wa miguu na shirikisho. Kwa bahati mbaya, hatutashiriki zaidi ya hapa”.
Mali itamenyana na wenyeji Cote d’Ivoire mnamo Februari 3 katika mchezo wa Robo Fainali na kuwa na nafasi ya kutinga hatua ya nne bora iwapo watashinda dgidi ya Tembo wa Afrika ya Magharibi.