Afisa Elimu Taaluma Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza, Samwel Kulinga (44) amefikishwa Mahakamani na kusomewa mashtaka manne likiwemo la kuendesha gari kwa mwendokasi, kuwagonga na kuwasababishia vifo watu watatu.
Akisomewa mashtaka hayo katika kesi ya trafiki namba 5383/2024 Januari 30, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kwimba, Dastan Ndeko, Wakili wa Serikali Frank Nchanila alisema shtaka lingine linalomkabili Afisa elimu huyo ni kuendesha gari bila ya leseni katika barabara ya Umma.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Wakili Nchanila aliwataja aliofariki kwa kugongwa na Afisa elimu huyo katika ajali iliyotokea Desemba 30,2023, eneo la Ilamba Wilayani Kwimba Mkoani humo kuwa ni mwendesha baiskeli, Shauri Masasi (62), Robert Matata (35), na Sara Faustine (43).
Alisema, “ukiwa unaendesha gari binafsi yenye namba ya usajili T. 374 EEV Toyota Wish kwa mwendokasi uliwagonga watumiaji wengine watatu wa barabara na kuwasababishia vifo kinyume na Kifungu namba 40 (1) na 63 (2) (a) cha Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 marejeo ya mwaka 2002.”
Mshitakiwa huyo, pia alidaiwa kutenda kosa la kuendesha gari kwenye barabara ya Umma bila leseni kinyume na Kifungu namba 52 (a) na 63 (2) (e) cha Sheria ya Usalama Barabarani sura namba 168 marejeo ya mwaka 2002, na aliachiwa baada ya kukidhi masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa kiongozi wa Serikali za mtaa.
Sharti lingine lilikuwa ni mdhamini atakayesaini bondi ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Shilingi 5 milioni na nakala ya Kitambulisho cha Taifa (Nida) ama Mpiga Kura, huku Hakimu akiahirisha shauri hilo hadi Februari 19, 2024, litakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kusomewa hoja za awali.